Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia anadi maeneo matano kuvutia uwekezaji nchini

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amehutubia Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg nchini Russia akihitimisha ziara yake ya siku tatu nchini humo, ambapo amenadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini akiwakaribisha Warussia kuja kuwekeza.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina sekta tano muhimu ambazo zinaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Rais Samia ameyasema hayo akihutubia Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg nchini Russia Ijumaa, Juni 5, 2026, akihitimisha ziara yake ya kikazi iliyodumu kwa siku tatu katika taifa hilo la katikati ya Ulaya na Asia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Jijini St. Petersburg nchini Urusi Juni 5, 2026. Kongamano hilo limewakutanisha Wafanyabiashara, Wawekezaji pamoja na Taasisi za kukuza Uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi.

Katika kongamano hilo lililoshirikisha zaidi ya wafanyabiashara 150 kutoka Tanzania na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali za Tanzania na Russia, Rais Samia ametaja pia juhudi zinazochukuliwa ili kuongeza fursa za ushirikiano wa kibiashara na kidiplomasia.

"Kwanza, Tanzania imebarikiwa aina mbalimbali za madini, yakiwemo dhahabu, uranium, nickel, graphite na madini mengine muhimu. Hivyo tunakaribisha ushirikiano wa utafiti na teknolojia za madini," amesema Rais Samia.

Ametaja sekta za kilimo, nishati safi, mafuta na gesi, pamoja na afya na vifaa tiba kama sekta muhimu za kushirikiana, akiweka wazi kuwa nia ya Serikali ni kuwezesha uzalishaji wa dawa za binadamu na wanyama kwa asilimia 60 kufanyika nchini ifikapo mwaka 2030.

"Tano, katika usafirishaji na ugavi, Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya bandari katika eneo la kimkakati la uchumi la Bagamoyo. Tunawakaribisha wawekezaji wa Russia kushirikiana nasi," amesema.


Rais Samia pia amesema Serikali inakusudia kuendeleza bandari ya Mangapwani visiwani Zanzibar, akisema upembuzi yakinifu tayari umefanyika. Katika sekta ya usafiri wa anga, amesema Shirika la Air Tanzania litaanza rasmi safari zake za Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow ifikapo Julai 2 mwaka huu, likiwa shirika la kwanza kufanya safari hizo.

Hatua hiyo ameitaja kuwa kichocheo muhimu cha kukuza na kuimarisha utalii baina ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Jijini St. Petersburg nchini Urusi tarehe Juni 5, 2026. Kongamano hilo limewakutanisha Wafanyabiashara, Wawekezaji pamoja na Taasisi za kukuza Uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi.

Akizungumzia umuhimu wa jukwaa hilo, Rais Samia amesema ni mpango muhimu katika kuwakutanisha wafanyabiashara wa kimataifa kujadili, kuonesha na kukuza biashara zao.

Ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania, Russia na bara la Asia katika jukwaa hilo wakionesha bidhaa zao, akiweka wazi nia ya Serikali kuendelea kuimarisha ushirikiano na taifa hilo.

"Huu ni wakati muafaka kwetu kuwekeza mkazo na kuwezesha ushirikiano mkubwa wa kiuchumi. Hali ya kibiashara kati ya nchi zetu kwa sasa haiendani na kiwango cha uhusiano wa mataifa yetu. Mwaka 2025 biashara kati ya mataifa yetu ilikuwa chini ya nusu bilioni ya dola za Marekani. Mwaka 2024 Russia ilikuwa na chini ya asilimia moja ya thamani ya mauzo ya nje. Hatupaswi kuwa hivi," amesema.

Rais Samia amesema Tanzania imefikia zaidi ya watu milioni 61, uchumi wake ukikua kwa asilimia 6 kwa mwaka na kuwa miongoni mwa nchi zenye ukuaji wa kasi barani Afrika.

Akizungumzia mchango wa miundombinu ya usafirishaji, ametaja Bandari ya Dar es Salaam ambayo imeunganishwa na reli ya SGR, ikihudumia zaidi ya nchi sita, kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi nchini.


Russia yaridhishwa na ujumbe wa Tanzania

Akizungumza baada ya hotuba ya Rais Samia, Waziri wa Biashara wa Russia, Maxim Reshetnikov, amesema mwingiliano wa wafanyabiashara wa Russia na Tanzania umeendelea kuimarishwa kupitia ushiriki katika majukwaa ya kibiashara ya kimataifa katika mataifa hayo.

"Ushirikiano wa wawekezaji na wajasiriamali wa Tanzania na Russia utaendelea wiki ijayo katika maonesho ya kimataifa hapa Russia na baadaye katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba nchini Tanzania," amesema.

Aidha, viongozi wa Russia wameeleza kufurahishwa na ushiriki wa Tanzania, wakiitaja kama taifa sahihi kwa uwekezaji na kuahidi kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kibiashara, huku wakipongeza ushiriki wa wafanyabiashara 150 kutoka Tanzania.

Wamepongeza pia hatua ya ATCL kutangaza safari za moja kwa moja kwenda Moscow, wakisema ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Jijini St. Petersburg nchini Urusi Juni 5, 2026. Kongamano hilo limewakutanisha Wafanyabiashara, Wawekezaji pamoja na Taasisi za kukuza Uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi.

Katika jukwaa hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Thabit Kombo, amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa Tanzania, akitaja mazungumzo yaliyofanywa na uwakilishi wa Russia nchini Tanzania kuwa yameibua fursa muhimu kwa Tanzania.

"Sisi Tanzania tupo tayari kufanya kazi nanyi katika maeneo ya kilimo. Rais Samia amekuja na zaidi ya wafanyabiashara 150 hapa Russia kama nyie mlivyowaleta Tanzania. Tupo tayari kwenye ICT, madini, sekta ya nishati, tupo tayari katika uongozi wa kidijitali na katika sekta ya utalii," amesema.


Mikataba ya ushirikiano yasainiwa

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari la BBC, Balozi Mindi Kasiga wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema ziara hiyo pia imeendeleza mahusiano mazuri yaliyojengeka kihistoria.

"Safari hii ni mpango uliokuwepo kwa muda mrefu, lakini pia imechochewa na mwaliko wa Rais mwenyeji, Vladimir Putin," amesema.

Akitaja malengo makuu ya ziara hiyo, amesema ni ziara ya kihistoria iliyolenga kuendeleza mahusiano ya nchi hizi kwenda hatua za juu zaidi, akitaja mikataba iliyosainiwa na mazungumzo yanayoendelea kwa wataalamu wa pande zote mbili kuhusu kuimarishwa kwa ushirikiano huo.

"Mojawapo ya mikataba ambayo imesainiwa ni katika nyanja ya elimu. Pia kwa masuala ya nishati mazungumzo yanaendelea," amesema.

Amefichua kuwa katika ziara hiyo kumekuwa pia na vikao vya mazungumzo ya wataalamu mbalimbali kutoka Tanzania na Russia kwa ajili ya kufanya uamuzi wa maeneo ya ushirikiano na mikataba inayosainiwa.

Amesema sera ya mambo ya nje ya Tanzania inayofuata mfumo wa kutofungamana na upande wowote inawezesha nchi kufungua uhusiano na nchi nyingi duniani, hatua muhimu inayoipa nchi fursa mbalimbali za kiuchumi na kidiplomasia.

Taarifa ya Ikulu kuhusu ziara hiyo ya kitaifa nchini Russia ilieleza kuwa safari hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo katika biashara, uwekezaji, nishati, madini, usafiri, elimu, teknolojia na utalii.

Rais Samia ameshiriki mazungumzo ya ngazi ya juu na Rais Vladimir Putin, Kongamano la Kimataifa la Uchumi la SPIEF 2026 na Jukwaa la Biashara Tanzania na Russia.

Katika sekta ya ushirikiano wa kiuchumi, taarifa inaonyesha kuwa MoU 23 tayari zimesainiwa kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi, huku rasimu nyingine 30 zikiwa katika hatua mbalimbali za majadiliano na MoU tano zikitarajiwa kusainiwa wakati wa ziara hii.

Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na nishati, gesi, nyuklia, uchimbaji madini, miundombinu, biashara na uwekezaji.

Aidha, mikataba muhimu iliyotajwa ni Makubaliano ya Huduma za Anga (BASA) ya mwaka 2024 yanayoruhusu safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Russia, MoU ya ushirikiano wa sekta ya usafiri iliyosainiwa Aprili 3, 2026, pamoja na MoU kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na BROKER VERSE DMCC/FESCO kuhusu maendeleo ya bandari na miundombinu ya reli.

Taarifa hiyo pia inabainisha kuwa Jukwaa la Biashara aliloshiriki Rais Samia linatarajiwa kuzalisha makubaliano mapya ya kibiashara na uwekezaji wa takribani dola bilioni 1.