Samia atunukiwa shahada ya heshima Russia, wadau wachambua uzito wake
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amefikisha shahada nane za heshima tangu aingie madarakani mwaka 2021, baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu nchini Russia, wachambuzi wakifafanua maana na uzito wa heshima hizo.
Dar es Salaam. Rais, Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Russia (RUDN University) jijini Moscow, nchini humo.
Tuzo aliyotunukiwa Rais Samia inaelezewa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika uongozi na maendeleo ya sekta mbalimbali na inaongeza rekodi yake ya heshima za kitaaluma nchini na kimataifa tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.
Hafla ya kutunukiwa shahada hiyo imefanyika chuoni hapo leo Alhamisi, Juni 4, 2026, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kitaifa nchini Russia ambapo Profesa Oleg Yastrebov, mhadhiri wa chuo hicho amesema: "Rais Samia amekuwa na mchango mkubwa katika uongozi, maendeleo ya kijamii, mageuzi ya sekta ya elimu, diplomasia ya kimataifa na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa yetu."
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Russia- (RUDN University) kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Profesa Oleg Yastrebov kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo Moscow nchini Russia, Juni 4, 2026.
Shahada hiyo inafanya idadi ya shahada za heshima alizotunukiwa Rais Samia kufikia nane, kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania.
Uongozi wa chuo kikuu cha RUDN umesema shahada hiyo imetolewa kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza maendeleo jumuishi, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, unaosaidia maendeleo ya elimu, afya na ustawi wa wananchi. Hafla hiyo imeongozwa na Rais wa Chuo hicho, Vladimir Filippov.
Akiwasilisha mada kuhusu ushirikiano kati ya Afrika na Russia, Profesa Oleg Yastrebov ameisifu Tanzania kwa hatua iliyopiga katika nyanja ya elimu, sayansi na teknolojia, huku akionyesha umuhimu wa heshima hiyo katika kuimarisha ushirikiano wa sekta ya elimu ya juu, sayansi, uwekezaji na teknolojia ya habari kati ya mataifa hayo mawili.
Safari ya shahada za heshima
Safari ya shahada za heshima kwa Rais Samia ilianza mwaka 2022 alipotunukiwa ya kwanza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Russia- (RUDN University) kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Profesa Oleg Yastrebov kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo Moscow nchini Russia, Juni 4, 2026.
Mwaka 2023, Rais Samia alitunukiwa shahada na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha India kutokana na juhudi zake za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya kijamii.
Mwaka huo huo, Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) kilimtunuku shahada kutokana na mchango wake katika usimamizi na masoko ya utalii.
Ilipofika mwaka 2024, Chuo Kikuu cha Ankara cha Uturuki, kilimtunuku shahada nyingine katika fani ya uchumi, kikafuatia Chuo Kikuu cha Korea Aerospace kilichotambua mchango wake kwenye maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga. Mwaka huo huo, Chuo Kikuu cha Mzumbe kilimtunuku Rais Samia shahada ya heshima katika uongozi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Russia- (RUDN University) kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Profesa Oleg Yastrebov kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo Moscow nchini Russia, Juni 4, 2026.
Chuo Kikuu cha Nasarawa State pia mwaka huu, kimetunuku shahada nyingine kutokana na mchango wake katika uongozi na diplomasia barani Afrika, kabla ya heshima ya RUDN University kumtunuku hii ya nane.
‘Ni kwa ajili ya Watanzania’
Akipokea heshima hiyo leo, Rais Samia amesema shahada aliyotunukiwa haihusu mafanikio yake binafsi, bali ni utambuzi wa mchango wa Watanzania wote katika maendeleo ya taifa na ushirikiano wa kimataifa.
“Naipokea kwa upole, kama Rais wa Tanzania, mtoto wa Afrika na rafiki wa Russia. Siipokei kwa ajili yangu, bali kwa ajili ya Watanzania,” amesema Rais Samia.
Amesema tuzo hiyo inakumbusha umuhimu wa elimu na maendeleo ya watu kama msingi wa uongozi bora.
Wachambuzi wazungumzia
Wachambuzi wa siasa, diplomasia na utawala bora wanasema kutolewa kwa mfululizo wa shahada za heshima kwa Rais Samia, kunathibitisha namna taasisi mbalimbali duniani zinavyotambua uongozi wake na nafasi ya Tanzania katika medani za kimataifa.
Mchambuzi wa masuala ya diplomasia, Hamduny Marcel, akizungumza na Mwananchi kwa simu amesema shahada hizo ni uthibitisho wa maendeleo yanayoonekana na mtindo wa uongozi unaolenga kusikiliza wananchi na kusukuma mbele maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Russia- (RUDN University) kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Profesa Oleg Yastrebov kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo Moscow nchini Russia, Juni 4, 2026.
Kauliu ya Marcel haiku mbali na maoni ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda aanayesema shahada za heshima hutoa utambuzi wa umahiri wa kipekee na zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia falsafa ya uongozi na athari zake kwa jamii.
Amesema kutunukiwa kwa heshima hii mpya kunahimiza uendelezaji wa diplomasia ya kimataifa ya Tanzania na kuendeleza historia ya jina la Rais Samia katika majukwaa ya elimu ya juu na diplomasia duniani.