Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi atoa kauli ishu ya Katiba mpya

Muktasari:

  • Asema katika eneo la utawala bora, Katiba mpya ndiyo msingi unaoweza kusimamia masuala mengine kwa kuwa sheria zinazopingana na Katiba zinaweza kubadilika au kuondolewa endapo kutakuwa na Katiba mpya yenye makubaliano mapana.



Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema jambo kubwa ambalo Watanzania wanapaswa kulipa kipaumbele katika mjadala wa mageuzi ya kisiasa ni kupatikana kwa Katiba mpya, akisema ndiyo sheria mama inayoweza kubeba na kusimamia masuala mengine yote ya utawala bora nchini.

Dk Nchimbi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), ambapo amesema endapo angepewa nafasi ya kuwaambia Watanzania jambo moja pekee, angewaomba kuendelea kupigania kupatikana kwa Katiba mpya yenye ridhaa ya wadau wote.

"Kama ningeambiwa Makamu wa Rais waambie Watanzania jambo moja tu, ningesema pambaneni mpate Katiba mpya. Katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote, Katiba yenye mwafaka katika taifa," amesema.

Dk Nchimbi amesema wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, aliwasilisha kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho maoni ya kamati ya ilani iliyokuwa imepewa jukumu la kukusanya maoni ya wananchi nchi nzima kuhusu mambo wanayoyataka, ambapo Katiba mpya ilikuwa miongoni mwa hoja kubwa zilizojitokeza.

Amesema baada ya kamati hiyo kumweleza kuwa Watanzania wanataka Katiba mpya, alisisitiza umuhimu wa suala hilo kupewa nafasi katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho, hasa kwa kuwa tayari kulikuwa na mgombea wa urais aliyekuwa akitarajiwa kuingia madarakani.

"Walipokuja kuniambia hilo nilimwambia mwenyekiti wa ile kamati na wenzake kwamba jambo lenyewe ni zuri, lakini tayari tuna mgombea wa urais na tunategemea atakuwa Rais, ni vizuri atuhakikishie," amesema.

Baada ya majadiliano hayo alikwenda kumuona aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kupata msimamo kuhusu kuingizwa kwa suala la Katiba mpya kwenye ilani ya chama.

"Nikamwambia mheshimiwa mwenyekiti, kamati ya ilani imekuja kuniona na moja ya mambo makubwa waliyobaini wananchi waliowatembelea ni kwamba wanataka Katiba mpya. Nikamuuliza, una utashi unataka jambo hili liingie kwenye ilani ya CCM?

"Akanijibu, Katibu Mkuu, Tume ya Haki Jinai niliyoiunda moja ya mapendekezo yake nayo ilibaini kwamba Watanzania wanataka Katiba mpya na niliwaahidi kwamba nitalitekeleza. Siwezi kuacha ahadi yangu," amesema.

Dk Nchimbi amesema kauli hiyo ilionyesha umuhimu wa kuwa na utashi wa kisiasa katika kushughulikia masuala makubwa ya kitaifa, akisisitiza kuwa mchakato wa Katiba mpya unahitaji ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.

Kufuatia hilo amewataka watetezi wa haki za binadamu, asasi za kiraia, vyama vya siasa na wananchi kutambua kuwa Katiba ndiyo sheria kuu ya nchi na hakuna sheria nyingine inayoweza kwenda kinyume nayo.

Akizungumza na watetezi hao amesema jitihada za kupata Katiba mpya zimekuwepo kwa zaidi ya miaka 40, huku mjadala huo ukiimarika zaidi baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

"Jambo la kwanza ni muhimu sana watetezi wa haki za binadamu, asasi za kiraia, vyama vya siasa na Watanzania kujua kwamba sheria kuu ya nchi ni Katiba. Hakuna sheria inayotengua Katiba," amesema.

Akizungumza kuhusu historia ya mchakato huo, Dk Nchimbi amesema katika Serikali ya Awamu ya Nne kulikuwa na hatua kubwa zilizopigwa baada ya kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya na kuundwa kwa Bunge la Katiba, lakini mchakato huo ulifikia hatua ukakwama.

Amesema katika harakati za kudai mabadiliko, Watanzania wanapaswa kuwa na mkakati wa kuchagua jambo muhimu zaidi litakaloweza kubeba madai mengine yote ya jamii.

"Tunaweza tukawa na mambo 40 ya kupigania, lakini katika mkakati wowote lazima uchague jambo kubwa ni lipi. Ukisikiliza madai mengi ya watu mbalimbali unakuta wamepanga mambo 10 kwa pamoja. Kushinda vita ya mambo 10 lazima uchague kubwa linaloweza kuyabeba mengine yote," amesema.

Amesema katika eneo la utawala bora, Katiba mpya ndiyo msingi unaoweza kusimamia masuala mengine kwa kuwa sheria zinazopingana na Katiba zinaweza kubadilika au kuondolewa endapo kutakuwa na Katiba mpya yenye makubaliano mapana.

"Ukipata Katiba mpya, sheria zote zilizopo zinazokinzana na Katiba hiyo siku hiyo hiyo zinakufa. Ndiyo maana Katiba ni jambo kubwa kuliko sheria nyingine yoyote," amesema.

Amesema Tanzania inahitaji Katiba itakayolinda haki za raia, kuheshimu utu wa binadamu na kuweka msingi wa maendeleo yanayozingatia maisha bora ya wananchi kwa miaka mingi ijayo.

"Katiba itakayotupeleka mbele miaka 50 inayokuja. Katiba ambayo kila Mtanzania popote alipo atajisikia fahari kujitambulisha kuwa anatoka Tanzania," amesema Dk Nchimbi.