VIDEO: Dk Tulia aeleza jinsi Bunge linavyomuelewa Rais Magufuli

Muktasari:

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema chombo hicho cha kutunga sheria kinamuelewa Rais John Magufuli  kutokana na miradi mikubwa anayoendelea kuitekeleza nchini.

Dar es Salaam. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema chombo hicho cha kutunga sheria kinamuelewa Rais John Magufuli  kutokana na miradi mikubwa anayoendelea kuitekeleza nchini.

Dk Tulia ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 26, 2019 wakati Rais Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika mradi wa kufua umeme wa Rufiji, mkoani Pwani.

“Huu ni moja ya miradi mikubwa uliyoanzisha sisi Bunge tumekuelewa na wananchi pia tunaowawakilisha wamekuelewa, jambo ambalo Bunge tunafurahi tunaposema ndiyo kule bungeni mambo tunaona yanatokea.”

“Zaidi ya Sh1 trilioni zimeshaingia, waliosema ndiyo wamefanikisha mradi huu, mawaziri wapo na wao huwa wanasema ndiyo, wanafanya kazi nzuri na wanawatumikia vizuri Watanzania, wapo wanaosema hapana wapo hapa lakini hata wao wanakuunga mkono kwa sababu ni sehemu ya bunge,” amesema Dk Tulia.

Amesema Bunge linaubeba uchumi wa viwanda kwa juhudi kubwa, “Tunashangaa wanaobeza, tunatazama treni, uchumi wa viwanda, wenyeviti wa kamati wapo hapa na watapeleka taarifa namna miradi hii yote inakusudia kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati na hakuna mradi ambao umesimama peke yake watakuelewa tu, bunge limekuelewa.”