Fatma Karume aibua utata mwaliko wake sherehe za Siku ya Sheria, Ikulu yamjibu

Fatume Karume


Muktasari:

Fatma, mwanaharakati wa sheria, alianzisha madai hayo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, akidai kuwa wamepigiwa simu na watu kutoka Ikulu ambao hakuwataja jina na kuambiwa kuwa awasilishe hotuba yake aliyopanga kuisoma siku hiyo, lakini asihudhurie.

Dar es Salaam. Utata umeibuka kuhusu waalikwa katika Siku ya Wanasheria itakayofanyika Februari 6 baada ya wakili maarufu jijini, Fatume Karume kudai kuwa kuna njama za kumzuia kushiriki licha ya kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Fatma, mwanaharakati wa sheria, alianzisha madai hayo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, akidai kuwa wamepigiwa simu na watu kutoka Ikulu ambao hakuwataja jina na kuambiwa kuwa awasilishe hotuba yake aliyopanga kuisoma siku hiyo, lakini asihudhurie.

Lakini mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa amesema madai hayo yanatakiwa kupuuzwa.

“Unataka mimi nithibitishe au nikanushe habari ambazo ziko hewani. Mimi sitafanya hivyo. Mwambieni yeye (Fatma) athibitishe hicho anachodai kinafanyika,” alisema Msigwa.

Katika akaunti yake ya Twitter, Fatma amedai jana kuwa kuna watu waliojitambulisha kuwa wanatoka Ikulu ambao wanaandaa mipango ya kutaka kuathiri ushiriki na uwepo wake katika sherehe hizo za kila mwaka.

Fatma alidai kuna maofisa waliompigia simu mtendaji mkuu wa TLS, Kaleb Gamaya wakimtaka afikishe ujumbe kwa Fatma kwamba hataruhusiwa kushiriki sherehe hizo.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Gamaya aliwataka wampigie simu Fatma kumfikishia ujumbe huo, lakini walisisitiza kuwa amfikishie.

Alisema maofisa hao walimpigia tena Gamaya, mara hii wakimwalika Ikulu kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa majaji wapya walioteuliwa na Rais.

Fatma anadai kwamba Gamaya alimjulisha kuhusu mwaliko huo na kumuuliza inakuwaje aende yeye (Gamaya) na wala si rais wa TLS. Lakini Fatma akamuomba Gamaya aende.

Katika ufafanuzi wake, Fatma alisema siku ya kuapishwa kwa majaji hao, Gamaya alifuatwa na watu ambao walimuuliza kama amepata simu kutoka Ikulu.

Fatma alisema Gamaya aliwauliza ni simu gani, akaelezwa ni kuhusu kumpa taarifa Fatma kuwa hataweza kuhudhuria sherehe za Siku ya Sheria. Alisema watu hao walisema kama Fatma atakuwa na hotuba ambayo angependa kuisoma siku hiyo, anaweza kumpa mtu mwingine afanye hivyo.

Kwa mujibu wa Fatma, Gamaya aliwaeleza kwamba Fatma ni lazima atahudhuria kwa kuwa tayari TLS walishapokea mwaliko rasmi kutoka Mahakama ambao kimsingi ndiyo wenye shughuli.

Alisema watu hao wakasisitiza kwamba Fatma apewe ujumbe wa kutohudhuria sherehe hiyo na kwamba kama Gamaya ana shaka amtafute Msajili Mkuu wa Mahakama, Katalina Revocati.

Alipoulizwa na Mwananchi, Katalina alithibitisha kutuma mwaliko huo, akisema hiyo ni desturi ya Mahakama kila mwaka inapoandaa sherehe za Siku ya Sheria.

Kuhusu kupokea maagizo kutoka Ikulu ya kumtaka atengue mwaliko huo, Katalina alisema hajapokea.

Lakini Mwananchi ilipotaka ufafanuzi wa madai ya Fatma, Gamaya alisema kilichosemwa na Fatma kinatosha.

Kuhusu nia ya kuhudhuria licha ya uwepo wa maagizo hayo, Fatma alisema: “Nitaenda kwa sababu kuna mwaliko rasmi wa Mahakama ambao ndiyo wenye sherehe yao.”