Gari la RC Mara lapata ajali likidaiwa kuendeshwa na mtoto wa dereva wake

Sunday August 4 2019

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Mara. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki amesema gari la mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima limepata ajali leo Jumapili Agosti 4, 2019 likiwa linaendeshwa na mtu anayedaiwa kuwa ni mtoto wa dereva wa mkuu huyo wa Mkoa.

Akizungumza leo Ndaki amesema ajali hiyo imetokea saa 3 asubuhi, kwamba gari hilo lenye namba za usajili STL 5961 lilikuwa likiendeshwa na mtu ambaye taarifa za awali zinaeleza kuwa ni kijana wa dereva wa Malima.

Hata hivyo, amesema bado hajapata jina la kijana huyo ambaye amesema kuwa amelazwa baada ya kupata majeraha.

Amebainisha kuwa baada ya uchunguzi wa ajali hiyo atatoa taarifa kamili, kwamba dereva wa gari hilo aliyemtaja kwa jina moja la Shida amelazwa katika hospitali ya Mkoa huo baada ya kupata mshtuko alipopokea taarifa za ajali.

Akizungumza na Mwananchi Malima amesema anasubiri taarifa ya polisi kuhusu ajali hiyo ili kujua chanzo ni nini.

“Ni kweli gari limepata ajali mimi nipo nyumbani sijaenda hata kuliona, nasubiri taarifa ya vyombo vya uchunguzi ili nijue kama kuna majeruhi niende kuwaona,” amesema.

Advertisement

Alipoulizwa lilipokuwa gari hilo Malima amesema, “Siwezi kusema lilikuwa na nani mpaka nipate taarifa kutoka kwa RPC (kamanda wa polisi wa Mara).”

 

Advertisement