Gramu 232 za heroine zawafikisha mahakamani Shamim Mwasha, mumewe

Muktasari:

  • Mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu kama Abdukandida (45) na mkewe Shamim Mwasha (41) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin.

Dar es Salaam. Mfanyabiadhara ,Abdul Nsembo maarufu Abdukandida (45) na mkewe Shamim Mwasha (41) ambao ni wakazi wa Mbezi Beach wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 232.70

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali, Costantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, alidai kuwa kosa lao ni la uhujumu uchumi.

Alidai kuwa Mei Mosi mwaka huu kwa pamoja washtakiwa hao wakiwa meneo ya Mbezi Beach walisafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 232.70 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kakula alidai upelelezi bado haujakamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mhina alisema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa kosa wanaloshtakiwa nalo ni la uhujumu uchumi hivyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na hawana dhamana.

Wakili wa utetezi, Hajra Mungula aliuomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili hatua nyingine ziweze kuendelea.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, 2019 itakapotajwa tena.