Halima Mdee apata dhamana, atakiwa polisi Februari 26

Mbunge wa Kawe Halima Mdee baada ya kupata dhamana katika kituo cha Polisi Osterbay alikoshikiliwa tangu jana.Picha na Fortune Francis

Muktasari:

  • Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) alikuwa akishikiliwa kituo cha Polisi Oysterbay tangu jana Jumamosi Februari 23, 2019 saa 2 asubuhi.

Dar es salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema),  Halima Mdee leo Jumapili Februari 24, 2019 saa 10 jioni amepata dhamana baada kushikiliwa kituo cha polisi Oysterbay kwa zaidi ya saa 24.

Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) alikuwa akishikiliwa kituoni hapo baada ya kuitikia wito wa mkuu wa upelelezi mkoa wa kipolisi Kinondoni (RCO) Jumamosi Februari 23, 2019.

Akizungumza na Mwananchi leo Hekima Mwasipu ambaye ni wakili wa Mdee amesema baada ya jana mbunge huyo kunyimwa dhamana aliendelea na taratibu mbalimbali kuhakikisha mteja wake anapata dhamana.

"Tumehangaika tangu jana lakini tunashukuru leo amepata dhamana ya polisi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili na kutakiwa kuripoti kwa mkuu wa upelelezi Februari 26,” amesema Hekima.

"Kwa kawaida mtuhumiwa hatakiwi kukaa kituoni kwa zaidi ya saa 24 kwa kuwa amepata dhamana tutarudi tarehe aliyopangiwa.”

Mdee amedhaminiwa na Hekima na mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Theonest.

Mdee anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano akidaiwa kusema: “Mtu ananunua ndege badala ya vifaa vya zahanati hii ni akili au matope.”