VIDEO: Hii ndiyo orodha ya viongozi wa dini matajiri zaidi Afrika

Uhuru wa kuabudu umezidi kutanuka Afrika, madhebu mbalimbalki ya dini yamekuwa yakianzishwa na kuungwa mkono.

Tanzania kwa mfano idadi ya madhehebu ya dini yameongezeka kwa kasi hususani katika miaka ya karibuni tofauti na ilivyokuwa enzi zile kina babu na bibi zetu walipokuwa wakipambana kusaka uhuru.

Huenda ongezeko hilo linatokana na mahitaji ya wakati au ni kutimia kwa maandiko ya vitabu vitakatifu vilivyoahidi kuibuka kwa imani nyingi na watumishi wengi wa imani za kidini.

Kuendelea kuongezeka kwa madhehebu ya dini sio tu kumechochea ungezeko la waumini bali pia kumeamsha ari ya upatikanaji wa ajira na kuongezeka kwa kipato.

Ongezeko hilo pia limeibua wachungaji wengi wenye kusikika na kusifika kutokana na huduma wazitoazo kuvutia wengi ndani na nje ya nchi zao.

Katika makala hii tunakuletea orodha ya mwaka 2019 ya wachungaji na watumishi wa dini waliotajwa na Jarida la Forbes la Marekani kuwa na utajiri mkubwa kutokana na kazi yao ya utumishi.

Mchungaji Chris Okotie (Nigeria)

Ni mmoja wa wachungaji maarufu wenye wafuasi wengi na mwasisi wa Kanisa la Household of God Church.

Aliwahi kusitisha masomo katika Chuo Kikuu cha Nigeria na kujihusisha na shughuli za muziki kisha kurejea chuoni na kuhitimu shahada ya sheria.

Baadaye alijiunga na Shule ya Biblia kisha kuanzisha kanisa lake. Pia amewahi kuwania urais wa nchi hiyo kwa mara kadhaa.

Anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia 10 milioni za Marekani (Sh23.3 bilioni) ambapo inaelezwa hutembelea magari ya kifahari kama Range Rover na Rolls Royce Phantom.

Mchungaji Matthew Ashimolowo (Nigeria)

Mchungaji Ashimolowo ana wafuasi wengi Afrika na nje ya bara hilo ambapo nchini Uingereza waumini 12,000 huhudhuria ibada katika kanisa lake kila Jumapili.

Aidha, anaendesha kipindi cha Njia za Ushindi “Winning Ways” kupitia vituo vya redio na televisheni mbalimbali Ulaya na Afrika.

Mchungaji Ashimolowo alijiunga na Ukristo akitokea katika Uislamu alipokuwa na umri wa miaka 20 baada ya kufariki baba yake.

Jarida la Forbes linakadiria utajiri wake kufikia Dola 10 milioni (Sh23.3 bilioni) huku kanisa lake likimiliki mali zenye thamani ya dola 40 milioni.

Ashimolowo amewahi kuchunguzwa na Tume ya Misaada ya England na Wales ambapo baadae ilitoa ripoti ikimtuhumu kwa matumizi mabaya ya fedha za miaada.

T.B. Joshua (Nigeria)

Temitope Balogun Joshua ni kiongozi maarufu wa kidini Afrika na dunia nzima akiwa na makao yake Nigeria.

Mmiliki wa kituo cha televisheni cha kikristo cha Emmanuel TV ambacho ni kikubwa pengine kuliko vyote Afrika.

Mbali na umaarufu wake kupitia tv hiyo, T.B. Joshua anawafuasi takribani milioni mbili katika mtandao wake wa Facebook huku akifuatiliwa na watu 800,000 katika chaneli ya YouTube wanaomfanya kuwa mchungaji maarufu zaidi. Jarida la Forbes limemkadiria utajiri wake kufikia dola 15 million (Sh34.9 bilioni).

Nabii Uebert Angel (Zimbabwe)

Mara nyingi husafiri kwa kutumia helkopta yake binafsi, ni rais na mwasisi wa huduma ya “Spirit Embassy”, iliyosajiliwa Uingereza na katika nchi mbalimbali. Amewahi kutajwa na moja ya majarida nchini humo kuwa nabii kijana mwenye karima na mhubiri mwanapanduzi.

Mwaka 2014 alitajwa na jarida la Forbes na kumfanya kuwa Mzimbabwe wa pili kutajwa katika jarida hilo.

Utajiri wake unakadiriwa kufikia dola 50 milioni (Sh116.6 bilioni), amethibitika kumiliki majengo ya makazi na biashara yenye thamani inayofikia dola 25 milioni.

Mchungaji Ray Mccauley (Afrika Kusini)

Mmoja wa viongozi wa dini maarufu zaidi Afrika Kusini. Awali alikuwa mchezaji wa mchezo wa kutunisha misuli na kuwahi kushiriki mashindano mbalimbali ya kiushindani kwa mchezo huo.

Baada ya kupata mafunzo ya Biblia, alianzisha kanisa la Rhema Bible Church ambalo sasa lina waumini zaidi ya 45,000 wanaolifanya kuwa miongoni mwa makanisa yenye nguvu nchini humo.

Amewahi kushutumiwa kutokana na maisha ya anasa na matumizi ya fedha nyingi zinzohusishwa na kanisa lake, lakini mwenye anasema anaisha kwa mshahara na kwamba anachotumia ni sehemu ya kile anachokipata kwa jasho lake. Utajiri wake ni dola 28 milioni (Sh65.3 bilioni).

Mchungaji Tshifhiwa Irene (Afrika Kusini)

Raia huyo wa Afrika Kusini na kiongozi wa Kanisa la Divine Truth World Restoration Services, ni miongoni mwa viongozi wa dini waliotengeneza mtandao imara kupitia mitandao ya kijamii na kuendelea kupata wafuasi wapya kila kukicha duniani kote. Utajiri wake unatajwa kufikia dola 42 milioni (Sh97.9 bilioni).

Mchungaji Chris Oyakhilome (Nigeria)

Chris Oyakhilome ni Rais wa huduma ya kikristo ya “Christ Embassy”.

Mchungaji Oyakhilome anaendesha kipindi cha televisheni kinachohusu kuamsha imani ambacho kimepata uungwaji mkono mkubwa na kufuatiliwa na mamilioni ya watu. Pia, ni mwandishi na mchapishaji vitabu mbalimbali vilivyotafsriwa katika lugha zaidi ya 140. Utajiri wake ni dola 50 milioni (Sh116.6 bilioni).

Askofu Ayo Oritsejafor (Nigeria)

Ayo Oritsejafor alikuwa Rais wa Shirikisho la Kikristo la Nigeria (CAN) ambapo amewahi kupokea tuzo mbalimbali kutambua mchango wake katika kuimarisha amani na usalama.

Kwa sasa ni kiongozi wa pili wa dini tajiri zaidi nchini Nigeria akimiliki ndege binafsi, chuo kikuuu (Eagles Height University) na benki. Utajiri wake ni dola 120 milioni.

Mchungaji Enoch Adeboye (Nigeria)

Kitaaluma ni Profesa wa hesabu aliyekuwa katika Chuo Kikuu cha Ilorin mpaka mwaka 1984 alipoamua kuachana na shughuli za kitaaluma na kujikita katika uchungaji.

Sasa ni kiongozi wa Kanisa la RCCG anayefanya kazi kubwa kulitanua na akupokea pongezi kutola pande mbalimbali. Kanisa lake lina matawi katika nchi 196. Utajiri wake unakadiriwa kuwa dola 130 za Marekani (Sh303.18 bilioni).

Askofu David Oyedepo (Nigeria)

Utajiri wake unakadiriwa kuwa dola 150 (Sh349.8 bilioni) anaongoza kanisa la Faith Tabernacle lililoanzishwa mwaka 1983 nchini Nigeria.

Akiwa kijana mdogo alidai kupokea ujumbe kutoka kwa Mungu uliomtaka kuisafisha dunia ambao aliamua kuufanyia kazi kwa kuanzisha kanisa ambalo sasa lipo katika orodha ya makanisa makubwa nchini humo. Mbali na uchungaji pia ni mwandishi wa vitabu. Kanisa lake linatajwa kumiliki majengo yenye thamani kubwa na ndege nne.

Nabii Shepherd Bushiri (Afrika Kusini)

Shepherd Bushiri ni mchungaji, mhubiri na mwasisi wa kanisa la Enlightened Christian Gathering lililo na waumini wengi Afrika Kusini na maeneo mbalimbali ya Afrika. Utajiri wake unakadiriwa kufikia dola milioni 150 (Sh349.8 bilioni).