Hilda wa Chadema amgomea RC Hapi

Mwanachama wa Chadema, Hilda Newton 

Muktasari:

Leo Ijumaa Desemba 21, 2018 saa 2. asubuhi, mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi alimtaka mwanachama wa Chadema, Hilda Newton kujisalimisha kwa kamanda wa polisi mkoa huo, Juma Bwire, hata hivyo mwanachama huyo amesema hatokwenda

Dar es Salaam. Mwanachama wa Chadema, Hilda Newton amesema hatokwenda kujisalimisha polisi mkoa wa Iringa, kama alivyotakiwa na mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi.

Hilda ametoa kauli hiyo jana jioni Alhamisi Desemba 20, 2018 wakati akizungumza na Mwananchi juu ya wito huo wa RC Hapi.

Desemba 18, 2018, RC Hapi alitoa agizo hilo kupitia ukurasa wake wa Twitter akimtaka Hilda kujisalimisha kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa, Juma Bwire leo Ijumaa Desemba 21, 2018 saa 2 asubuhi.

Agizo hilo lilitokana na kile kinachodaiwa kuelezwa na Hilda kwamba mkuu huyo wa mkoa mwezi mmoja uliopita alilazwa nje katika makaburi na watu wasiojulikana.

Hilda  akizungumzia wito huo wa RC Hapi alisema, “Kama anahisi kakosewa akafungue kesi halafu polisi ndo wanitafute.”