VIDEO: Hivi ndivyo Mbowe alivyomzungumzia Lowassa

Muktasari:

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe leo Ijumaa amemzungumzia aliyekuwa mgombea urais wa Chadema mwaka 2015, Edward Lowassa ambaye Machi Mosi, 2019 alitangaza kurudi CCM

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kuondoka kwa mwanachama wake Edward Lowassa kwenda CCM huku akimtaka kusema ukweli huko aliko.

Mbowe akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Machi 15, 2019 jijini Dar es Salaam amesema, “Chama cha siasa, Mwalimu Nyerere alizungumza wakati wa uhai wake, akisema chama cha siasa ni dodoki, kwamba ukiliweka kwenye maji litanyonya maji, ukiliweka kwenye maziwa litanyonya maziwa.”

“Sisi kama chama cha siasa ni wajibu mkubwa katika kukijenga chama na kuongeza wana chama na katika mkakati huohuo tulimwongeza Lowassa mwaka 2015.”

Mbowe amesema, “Lakini ambalo nataka kulizungumza kwa kifupi sana, vyama vyetu vinavuta watu wa makundi mbalimbali kwa sababu mbalimbali.”

Amesema wako watu wema, wako wasio wema, wako pengine kwa kupenda madaraka, wako watu wanatumwa kuwatumikia watu.

“Kila mmoja katika uelewa wake ana wajibu wake wa kutambua anataka nini na ndani ya Chadema kila mmoja ana malengo yake japo tunakuwa na malengo yanayofanana,” amesema.

“Kupinga uovu, kuihubiri haki na kulaani yasiyo na mashiko, katika kulifanya hili inahitajika wajibu na kazi hii ni ngumu, wako tulioanza nao wakashindwa katikati, wako tuliowakuta katikati wameshindwa na tumewaacha na kila mmoja na sababu yake,”  amesema.

Amesema ila kwa sababu lengo letu ni kuisimamia haki kupitia demokrasia, naamini ni bora asiwepo.

“Nilisikitika, nikisema nafurahi nitakuwa mwongo, lakini kwenda katika chama kingine cha siasa basi akaseme kweli na itusaidie kwamba chama chake kipya kisiendelee kuwatesa na mjadala huu naufungia hapo,” amesema Mbowe na kuongeza kuwahawatajenga chama chenye visasi na Chadema si chama cha visasi.