Hivi ndivyo wanavyotunzwa washindi, washiriki mashindano ya Qur’an

Juzi zilifanyika fainali za mashindano maalumu ya 20 ya kuhifadhi Qur’an yaliyoshirikisha washiriki 20 kutoka mataifa 18 ya Afrika.

Mashindano maalumu ya 20 ya kuhifadhi Qur’an yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma yalifanyika katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi waliojuaza uwanja huo huku wengine wakilazimika kwenda kusikiliza matangazo ya moja kwa moja kwenye uwanja wa Uhuru baada ya Taifa kujaa na maofisa usalama kuzuia.

Mbali na maelfu ya watu hao, pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo, Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, marais wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete, makamu wa rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir, Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda na mabalozi wa nchi mbalimbali.

Waislamu sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuhifadhi Qur’an kwa kuwa kitabu hicho pamoja na mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW) ndiyo msingi mkuu unaofuatwa katika kutekeleza mambo mbalimbali kwenye maisha ya Muislamu.

Mashindano ya Qur’an mara nyingi hufanyika katika mwezi wa Ramadhani kwa kuwa ndio mwezi kitabu hicho kitukufu kilipoteremshwa kupitia Mtume Muhammad (SAW) kwa kipindi cha miaka 23, miaka 13 akiwa Makka na 10 akiwa Madina nchini Saudi Arabia.

Kwa kipindi cha miaka 20 bila shaka wanaoyafuatilia mashindano hayo tangu yalipoanza mwaka 2000 hapa nchini watakuwa wanajiuliza washindi na washiriki wa michuano hiyo hasa kutoka Tanzania wanaendelezwaje au kusaidiwaje baada ya mchakato huo unaofanyika kwa mwaka mara moja kukamilika.

Miongoni mwa malengo ya mashindano hayo ni pamoja na kuwafanya vijana wa Kiislam kukijua vyema kitabu hicho kitufuku sanjari na kuwajenga katika maadili mema.

Sheikh Kishk afafanua

Gazeti hili lilifanya mahojiano na mwenyekiti wa mashindano hayo, Sheikh Nurdin Kishki ambaye anaeleza namna wanavyoendelezwa washindi na washiriki wengine na kusaidiwa katika kuhakikisha wanaendeleza kipaji chao cha kuhifadhi Qur’an.

Sheikh Kishki ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Al-Hikma anasema washiriki wanaopitia kwenye taasisi hiyo wanapewa majukumu ikiwamo kuwaendeleza kielemu ili kujikomboa kimaisha.

“Mfano mshiriki au mshindi ametoka Al-Hikma amemaliza darasa la saba, tunamsomesha katika shule zetu.

Akimaliza tunamuuliza anataka kusoma fani gani kama ualimu tunampeleka chuoni na akihitimu tunampatia ajira ya kufundisha kwenye shule zetu,” anasema Sheikh Kishki.

Kwa mujibu Sheikh Kishki, tangu mashindano yaanze, zaidi ya washiriki 20 waliopitia taasisi hiyo wamesaidiwa katika masuala mbalimbali ikiwamo kielimu na kuwapatia darasa maalumu la kufundisha Qur’an na kulipwa.

“Siyo hilo tu, pia tumewasaidia kuwatafutia mashindano mengine kama haya katika nchi za Uturuki, Misri na Saudi Arabia. Wale washiriki au washindi Watanzania wanaotoka nje huwa tunawaita wao na walimu wao na kuzungumza nao na kuwapa ushauri wa namna wanavyoweza kushirikiana nao katika masuala mbalimbali,” anasema Sheikh Kishki.

Vivyo hivyo, kwa washiriki wanaotoka nje ya Tanzania huwaita na kukaa nao pamoja kwa ajili ya kuzungumza masuala mbalimbali ya namna watakavyoweza kuelendeleza vipaji vyao vya kuhifadhi.

Hata hivyo, Sheikh Kishki anasema katika suala la kuhifadhi la Qur’an wazazi wenye watoto Waislam wamekuwa na mchango mdogo wa kushiriki katika mchakato huo.

“Baadhi ya wazazi hawaungi mkono suala hili, sehemu kubwa tunasimamia wenyewe. Utakuta mzazi hajishughulishi kabisa, lakini akisikia mwanaye amepata zawadi ya Sh10 milioni ndio anajitokeza.

“Hata hivyo, sasa kumekuwa na mwamko kidogo baada ya mashindano haya kuzidi kukua na kutangazwa zaidi kwenye vyombo vya habari,” anasema.

Yalivyomfurahisha JPM

Katika mashindano hayo Rais Magufuli hakusita kueleza hisia zake kuhusu mchakato huo akisema amekuwa akiyafuatilia kwa ukaribu, licha ya kutoelewa kinachozungumzwa wakati washiriki hao wakisoma Qur’an lakini sauti zao zilimvutia zaidi.

Akionekana mwenye furaha wakati wote, Rais Magufuli anasema umati uliojitokeza katika mashindano hayo katika uwanja huo unaochukua takribani watu 60,000 inaonyesha namna ambavyo masuala ya Mungu yanamgusa kila mtu bila kujali tofauti za dini.

“Siku nyingi tumezoea tukija katika uwanja huu, hasa zinapokutana timu kubwa za Yanga na Simba utaona wanavyoshangilia, lakini leo (juzi), tumekusanyika hapa kwa umoja wetu kumshangilia Mungu kwa ajili ya kitabu chake kitukufu cha Qur’an, nimefurahi sana,” anasema Rais Magufuli huku akishangiliwa kwa nguvu na umati huo.

Mkuu huyo wa nchi alitumia fursa hiyo kuzungumza na Waziri Nchi, na mjumbe wa baraza la mawaziri Saudi Arabia, Dk Saleh Alashiek aliyekaa naye katika jukwaa kumweleza nia yake ya kutaka kujengwa kwa Chuo Kikuu cha Kiislam nchini.

Akiwa katikati ya hotuba yake, Rais Magufuli alitoboa siri ya mazungumzo yake na Dk Alashiek akisema alimchomekea waziri huyo kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kiislam hapa Tanzania kitakachofadhiliwa na Saudi Arabia.

“Amenihakikishia waziri (Dk Alasheikh) kuwa atakwenda kumueleza mfalme wa Saudi Arabia na katika hatua za kwanza mfalme ameonyesha nia ya kukubali kujenga chuo hiki mapema kwa niaba yenu ndugu zangu Waislam na Watanzania. Napenda nimshukuru sana Dk Alashiek na mfalme kwa niaba ya Watanzania wote,” anasema Rais Magufuli.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete akizungumza katika mashindano hayo alisema ujio wa Rais Magufuli katika mashindano hayo ni faraja kubwa hasa maneno mazuri aliyoyasema ya kusisitiza mshikamano baina ya Watanzania.