VIDEO: Hukumu kesi ya Malkia wa Tembo Februari 19

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 19, 2019 kutoa hukumu katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu, akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan(66).


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Februari 19, 2019 kutoa hukumu katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu, akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66).

Glan, maarufu kama Malkia wa Tembo na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni, kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo ilitakiwa kutolewa leo, Februari 15, 2019 lakini Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, anayesikiliza shauri hilo bado hajamaliza kuandika hukumu.

Hakimu Shaidi amesema, kuna vitu anamalizia kuviandaa katika hukumu hiyo, hivyo amepanga Jumanne ya wiki ijayo ndio atatoa hukumu.

"Nitatoa hukumu hii siku ya Jumanne ya wiki ijayo, kuna vitu namalizia katika uandikaji wa hukumu hii," alisema Hakimu Shaidi.

Awali, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akisaidiwa na Salim Msemo, amedai leo Februari 15, 2019 kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya hukumu na wapo tayari kwa hilo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi alisema kuwa atatoa hukumu hiyo, Februari 19, 2019 na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Mbali na Glan, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase, ambao wote wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Hassan Kiangio.

Hukumu huyo inatarajia kutolewa baada mahakama hiyo kuwakuta washtakiwa hao na kesi ya kujibu.

Hatua hiyo inatokana na upande wa mashtaka kupelekea mashahidi 11 waliotoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa katika kipindi hicho walifanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889, vikiwa na thamani ya Sh13bilioni bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na mkurugenzi wa wanyamapori.