Huu ndio msimamo wa CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad

Muktasari:

  • Januari 21 ndio siku ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG) Profesa Mussa Assad atakapohojiwa na Kamati ya Maadili Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge hiyo ni baada ya kuieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa Bunge halifanyi kazi yake kama linavyotakiwa na kwamba ni matarajio yake kwamba udhaifu huo utarekebishwa.


Dar es Salaam. Zimebaki siku tisa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusimama mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma za kuudhalilisha mhimili huo wa Dola wa kutunga sheria.

Kitendo hicho kitamfanya Profesa Assad aandike historia ya kufikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya kamati hiyo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Desemba Mosi, 2014.

Mtaalamu huyo wa uhasibu na ukaguzi anafikishwa mbele ya kamati hiyo, baada ya kuieleza idhaa ya Kiswahili ya kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Bunge halifanyi kazi yake kama linavyotakiwa na kwamba ni matarajio yake kwamba udhaifu huo utarekebishwa muda si mrefu.

Alikuwa akijibu swali la mtangazaji wa kituo hicho, Arnold Kayanda kuhusu kutotekelezwa kwa mapendekezo anayotoa kwenye ripoti zake, hasa kuhusu ufisadi.

“Kama tunatoa ripoti na kuna ubadhirifu na hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa lisimamie na kuhakikisha kwamba pale penye matatizo, linahakikisha kuwa hatua zinachukuliwa. Sasa, sisi kazi yetu ni kutoa ripoti tu,” alijibu.

“Na huo udhaifu, nafikiri ni jambo la kusikitisha, lakini ni jambo ambalo tunaamini muda si mrefu litarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa. Na sitaki kuwa labda nasema jambo hili kwa sababu linahusisha watu fulani, hapana. Lakini nafikiri Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata udhaifu ambao unaonekana, utakwisha.”

Swali hilo ndilo liliifanya Mwananchi ifanye upekuzi katika baadhi ya ripoti za CAG ambazo zinaweza kuwa ndizo zilizomfanya Profesa Assad atoe maoni hayo kuwa Bunge halitekelezi wajibu wake ipasavyo.

Hadi sasa, Profesa Assad ameshatoa ripoti mbili na katika utangulizi wa ripoti hizo zote (ya mwaka 2015/16 na ya 2016/17), ameeleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa maoni ya ukaguzi, akibainisha baadhi ya mambo ambayo kamati za Bunge (ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) na Hesabu za Serikali (PAC), zilitakiwa kuyafanyia kazi baada ya kuzipokea.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiambia Mwananchi kuwa hawezi kuzungumzia maoni hayo yaliyo kwenye ripoti hizo mbili hadi hapo Profesa Assad atakapohojiwa Januari 21, lakini akasema anao ushahidi wa maandishi kuthibitisha kuwa chombo chake kinatekeleza wajibu kilichopewa na umma.

Katika ripoti ya mwaka 2015/16, CAG anaeleza kuwa hali ya utekelezaji wa mapendekezo ya ofisi yake ilikuwa asilimia 14 pekee.

“Hali ya utekelezaji wa mapendekezo hayo hairidhishi, kwani kati ya mapendekezo 234 yaliyotolewa ni mapendekezo 32 (asilimia 14) yametekelezwa kikamilifu,” inasema ripoti hiyo iliyosomwa Machi 2017.

Katika ripoti hiyo, pamoja na mambo mengine, ilionyesha kasoro mbalimbali katika taasisi na mashirika ya umma ambazo zilisababisha Serikali kupoteza mapato na kupata hasara kutokana na uzembe wa watendaji.

Ripoti ilieleza namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilivyokuwa na matumizi mabaya ya misamaha wa kodi ya Sh3.46 bilioni pamoja na usimamizi na ufuatiliaji usioridhisha wa madeni ya kodi na tozo zinazofikia Sh613.6 bilioni.

Pia, ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na utekelezaji hafifu wa bajeti kwa asilimia 6.16 ya makisio pamoja na kuongezeka kwa Deni la Taifa kwa asilimia 22.

Kuhusu matumizi mabaya ya fedha serikalini, “Ukaguzi wangu umebaini matumizi yasiyokuwa na manufaa ya jumla ya Sh1.46 bilioni kwa Serikali Kuu. Matumizi haya yangeweza kuepukwa endapo taasisi husika zingekuwa makini,” inasema ripoti hiyo.

Katika mapendekezo yake, CAG aliishauri Serikali kuhakikisha inatekeleza kikamilifu mapendekezo mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utendaji wake.

Pia, ripoti ya mwaka 2016/17 iliyotolewa Machi mwaka jana ilizitaja taasisi za umma zilizokutwa zikiwa zimetumia vibaya fedha. Taasisi zilizotajwa na CAG ni pamoja na TRA, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Katika ripoti hiyo, utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ulionekana kutoridhisha. Kati ya mapendekezo 201 yaliyotolewa katika ripoti zilizopita, ni mapendekezo 43 sawa na asilimia 21 yaliyotekelezwa kikamilifu.

“Mapendekezo 103 (sawa na asilimia 52), utekelezaji wake unaendelea, na mapendekezo 55 sawa na asilimia 27 utekelezaji wake haujaanza,” inasema ripoti hiyo.

Serikali za mitaa zilitekeleza kwa asilimia tano na Serikali Kuu kwa asilimia 29 huku mashirika ya umma ni kwa asilimia 31.

Profesa Assad anasema katika ripoti hiyo kuwa, TRA kulikuwa na upungufu unaotokana na kesi za muda mrefu zilizopo mahakamani ya kodi zinazofikia Sh4.4 trilioni na upungufu katika kushughulikia mapinganizi za kodi zinazofikia Sh739 bilioni.

Ripoti hiyo pia inasema udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa mizigo inayopita nchini kwenda nje ulisababisha lita milioni 26 za mafuta ambayo kodi yake ni Sh14 bilioni kutumika ndani ya nchi badala ya kusafirishwa kwenda nje kama ilivyokusudiwa na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

CAG pia alipendekeza kuboreshwa kwa njia za ukusanyaji wa mapato, hasa kwa Serikali za Mitaa pamoja na kutoa fedha za ruzuku ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Laac, Vedasto Mwiru hakutaka kuzungumzia suala hilo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mapendekezo yaliyo kwenye ripoti hizo, hadi sakata hilo litakapoisha.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye aliwahi kuiongoza PAC, alisema kusuasua kwa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti za CAG ni kikwazo kwa CAG.

“Hizo takwimu zinathibitisha maneno na manung’uniko ambayo CAG amekuwa nayo,” alisema.

“CAG si polisi wala si Takukuru. Wanaopaswa kufuatilia utekelezaji wa hayo mambo ni Bunge kupitia kamati zake. Kwa hiyo kama kamati hazifanyi kazi CAG atakuwa anaandika ripoti tu,” alisema.

Kiongozi huyo wa Chama cha ACT alitetea kauli aliyotoa Profesa Assad katika mahojiano hayo ni kituo cha UN.

“CAG hakusema Bunge ni dhaifu, alisema ni udhaifu wa Bunge. Kwa hiyo Spika amechukua hatua kwa jambo ambalo ni maoni tu,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa Profesa Assad au ofisi ya CAG kulikumbusha au kulilalamikia Bunge kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa kwenye ripoti za ukaguzi.

Wakati alipoulizwa kuhusu ripoti yake iliyoonyesha kuwa Sh1.5 trilioni za bajeti ya mwaka 2016/17 hazikukaguliwa, Profesa Assad alisema suala hilo linapaswa kuhojiwa na Bunge kwa kuwa jukumu lake (CAG) ni kutoa ripoti tu.

CAG aliyepita, Ludovick Utouh alisisitiza kila mara katika ripoti zake kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, hadi Rais John Magufuli alipolishughulikia baada ya kuingia madarakani mwaka 2015.