Huu ndio msimamo wa Chadema, uchaguzi wa ubunge ‘jimbo la Nassari’

Muktasari:

  • Jana, akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Jaji Kaijage alisema NEC ilipokea barua kutoka kwa Spika Ndugai ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi aliitaarifu kuwapo kwa nafasi ya ubunge iliyo wazi katika jimbo hilo.

Dar/Moro. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitangaza uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki kufanyika Mei 19, Chadema kimesisitiza msimamo wake wa kutoshiriki mpaka mwaka 2020.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimetoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage kutangaza tarehe ya uchaguzi huo.

Uchaguzi utafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Joshua Nassari wa Chadema ambaye amepoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.

Machi 14, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuandikia barua mwenyekiti wa NEC kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na mbunge wake kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.

Mikutano ambayo Nassari hakuhudhuria ni wa 12 uliofanyika Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, wa 13 uliofanyika kuanzia Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na wa 14 ulioanza Januari 29 hadi Februari 9 mwaka huu.

Hata hivyo, Nassari hakukubaliana na uamuzi huo hivyo akafungua kesi Mahakama Kuu ambayo baada ya kusikiliza pande zote, Alhamisi iliyopita ilitoa hukumu ‘iliyopigilia msumari’ kilichofanywa na Spika Ndugai dhidi yake.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Jaji Kaijage alisema NEC ilipokea barua kutoka kwa Spika Ndugai ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi aliitaarifu kuwapo kwa nafasi ya ubunge iliyo wazi katika jimbo hilo.

“Nafasi ya Jimbo la Arumeru ipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge, Joshua Samwel Nassari kupoteza sifa kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika,” alisema Jaji Kaijage,

Alisema fomu za wagombea zitatolewa kuanzia Aprili 15 hadi 19 na uteuzi wao utafanyika Aprili 19 kabla kampeni za uchaguzi hazijaruhusiwa kuanzia Aprili 20 hadi Mei 18.

Alivitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.

Alipotafutwa kutoa maoni yake kuhusu taarifa hiyo ya NEC, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema “hatujabadili msimamo wa chama kutoshiriki chaguzi hizi, kwa sasa mtazamo wetu ni uchaguzi mkuu.”

Alipoulizwa ikiwa Nassari mwenyewe atataka kugombea tena, mtendaji huyo mkuu wa Chadema alijibu, “chama ndicho kinachoamua, chama kiko juu ya mtu na mtu hayuko juu ya chama.”

Aidha, alipoulizwa endapo Nassari atataka kuwania tena nafasi hata ikibidi kupitia chama kingine, Dk Mashinji alisema kinachomweka mtu kwenye chama ni itikadi, “lakini kama ana kuwa ndani ya chama kwa ajili ya madaraka anaweza kuondoka.”

Dk Mashinji pia alijibu swali kuwa kilichotokea kwa Nassari ni uzembe wa chama kutofuatilia wabunge wake kujiridhisha kama wanahudhuria bungeni, alisema si kweli, bali wamekuwa wakifuatilia mienendo yao.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alipoulizwa kama watashiriki uchaguzi huo alisema, “Hilo ni eneo la Chadema. Mbunge alikuwa Chadema wana haki ya kuweka mgombea. Hatutaweka mgombea na badala yake tutaunga mkono mgombea wa Chadema.”

Alipoelezwa kwamba Chadema imetoa msimamo wa kutoshiriki uchaguzi huo, alisema, “tutaunga mkono uamuzi wa Chadema.”

Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman alisema wataitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji kujadili kama watashiriki katika uchaguzi huo au la.