Huyu ndiye Rais Bongo wa Gabon aliyenusurika kupinduliwa

Vijana watano walioasi katika Jeshi la Gabon juzi walizua kizazaa baada ya kutangaza kuipindua Serikali ya Rais Ali Bongo ambaye mwaka 2016 alianza muhula mpya wa kuiongoza nchi hiyo baada ya ushindi mwembamba kupitia uchaguzi mkuu.

Katika taarifa ya mapinduzi hayo iliyotolewa alfajiri ya siku hiyo na kiongozi wa mapinduzi, Luteni Kelly Ondo Obiang, kupitia redio ya taifa, vijana hao walidai uamuzi huo unalenga kurudisha utawala wa kidemokrasia Gabon.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye Msemaji wa Serikali, Guy-Bertrand Mapangou alijitokeza na kusema hakuna yeyote aliyempindua Rais Bongo na Serikali yake na kwamba kila kitu kipo chini ya uangalizi salama.

“Hali ni tulivu. Vikosi vya usalama vinadhibiti na kulinda eneo la makao makuu ya televisheni na redio ya taifa. Kila kitu kimerejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Mapangou. Alisema yeyote aliyetajwa katika taarifa ya waasi hao awe ni jenerali, kiongozi wa upinzani au wa chama cha kijamii, atachunguzwa.

Jaribio la mapinduzi hayo limefanyika huku Rais Bongo akiwa nchini Morocco kwa miezi miwili sasa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa kiharusi.

Taarifa ya Ikulu ilisema watu wawili kati ya walioshiriki mapinduzi hayo yaliyofeli wameuawa katika majibizano ya risasi pale vikosi vya Serikali vilipokuwa vikizirudisha studio hizo katika uangalizi wao.

Mbali na waliouawa, wengine watatu wanashikiliwa akiwemo Luteni Obiang aliyechomolewa uvunguni alikojificha baada ya kufeli kwa mapinduzi hayo.

Upinzani unasemaje?

Muungano wa vyama vya upinzani umekana kuhusika kwa namna yoyote katika mapinduzi hayo. Hata hivyo, ulisema unajua sababu ya jeshi kutaka kuipindua Serikali lakini haukuziweka wazi.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa muungano wa vyama vya upinzani nchini humo, Laurence Ndong, alisema wanaelewa kwa nini wanajeshi hao walijaribu kupindua Serikali.

Awali mmoja wa viongozi wa muungano huo, Paul-Marie Gondjout, alisema hawafahamu lolote zaidi ya kusikia kilichotokea na kushuhudia vikosi vya ulinzi na polisi wakifanya ukaguzi mkali katika vizuizi vya barabarani. “Tumesikia agizo na kauli ya Serikali lakini hatufahamu chochote”.

Alisema kwa kuwa Rais Bongo hayupo nchini humo kwa miezi miwili sasa, makamu wake anapaswa kuapishwa ili kushikilia madaraka ya nchi. “Nchi lazima iwe na utawala, lakini hatuna Serikali wala kiongozi mkuu wa Serikali”.

Jinsi jaribio la mapinduzi lilivyofanyika

Waasi hao waliteka redio na televisheni ya taifa saa 10.30 alfajiri kisha Luteni Obiang alisoma taarifa fupi ya mapinduzi.

Sehemu ya taarifa iliyosomwa na Obiang ilisema. “Kama unakula acha, kama unakunywa acha, kama umelala amka na uwaamshe majirani zako…simameni pamoja kushika hatamu mtaani kwenu”.

Tamko hilo liliibua vurugu mitaani ambako vijana walijitokeza na kuzuia magari na kuchoma matairi.

Mji mkuu Libreville uligubikwa na ukimya huku shughuli mbalimbali zikisimama, maduka kufungwa na mashirika ya kimataifa yakiwatangazia watumishi wake kutotoka nyumbani.

Walioshiriki jaribio hilo walifanikiwa kuingia studio hizo baada ya kuwadhibiti walinzi wa ofisi hizo.

Hata hivyo, vikosi vya Serikali baadaye viliwadhibiti waasi hao ikiwamo kuwapiga risasi na kuwaua wawili kati yao na kurudisha uangalizi wa redio na televisheni hiyo katika mikono salama.

Inaelezwa kuwa jaribio hilo limefanyika kwa kushitukiza wakati ambapo mfumo wa ulinzi wa rais na jeshi la nchi hiyo ukiongozwa na watu walio watiifu kwa Rais Bongo.

Vijana watatu waliovalia kijeshi walionekana kupitia video iliyosambaa mitandaoni wakitangaza mapinduzi hayo lakini muda mfupi baadaye Luteni Kelly Ondo Obiang aliyejitambulisha kuwa ni kutoka jeshi la nchi hiyo aliwataka askari wote kuendelea na kazi katika maeneo waliyopangiwa.

Gabon inaungana na nchi nyingine za Afrika zilizozima mapinduzi miaka ya hivi karibuni za Benin (2013), Burkina Faso (1983 na 1989), Burundi (2015), Cameroon (1984) Afrika ya Kati (2013), Chad (2013), Comoro (2013) Equatorial Guinea (2004), Gambia (2014), Lesotho (2014), Libya (2016) na Mali (2012).

(Imeandaliwa na Suleiman Jongo kwa msaada wa mitandao)