Ijue Kinga dhidi ya radi

Muktasari:

  • Mtaalamu wa radi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) amesema upepo mkali na wingu zito ni dalili ya kuwapo kwa radi hivyo hali hiyo inatosha kwa mtu kuchukua tahadhari.

Dar es Salaam.  Wakati radi ikiua watu sita ndani ya siku tatu mkoani Tabora, mtaalamu wa radi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Wilberforce Kikwasi amesema wananchi wanaweza kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yake.

Akizungumza na Mwananchi Digila, Kikwasi amesema radi ni umeme mkubwa unaotoka mawinguni kuja ardhini hivyo dalili za kuwapo kwake kipindi cha mvua huwa zinajulikana.

“Radi huwa inakuja na wingu zito jeusi linalombatana na upepo mkali kwa hiyo hata kama ukiwa shambani unalima ukiona dalili hizi ni vizuri uchukue hatua kuepuka madhara ya radi,” amesema.

Ameeleza kuwa mara nyingi dalili za radi zinaweza kuonekana wakati watu wapo kwenye majukumu mbalimbali hivyo ni vizuri kuchukuwa tahadhali ili kuepuka madhara yake,

Mtaalamu huyo amesema shamba au kuwa kwenye eneo tambarare lisilo na nguzo, nyumba wala miti ni hatari zaidi kwa sababu binadamu huwa mrefu kuliko kitu kingine na kwamba radi ina tabia ya kutua kwenye kitu kirefu zaidi ndipo ifike ardhini.

“Ukiwa eneo hilo wewe ndio unakuwa mrefu zaidi kuliko kitu kingine chochote na ukiona hivyo unashauriwa kutafuta sehemu salama kujikinga na radi,’ amesisitiza Kikwasi.

Amesema mtu akiona ni vigumu kwenda mbali, anatakiwa kuchuchumaa na kuinamisha kichwa kwenye mapaja.

Anashauri mtu akiwa kwenye maeneo yenye miti hapaswi kusimama chini yake kwa sababu ni hatari kwa kuwa radi inaweza kupiga mti huo naye akapata madhara.

“Usipende kukimbia haraka kwenye kujikinga mvua chini ya miti kwa sababu unaogopa kulowana, radi inaweza kupita kwenye huo mti na ikakujeruhi hivyo ni bora ukae mbali na miti,” amesema.