Jacqueline Mengi amshukuru Rais Magufuli

Muktasari:

  • Jacqueline Ntuyabaliwe, mjane wa  Reginald Mengi amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli na viongozi mbalimbali walioshiriki msiba wa mumewe aliyefariki dunia Mei 2, 2019

Dar es Salaam. Jacqueline Ntuyabaliwe, mjane wa  Reginald Mengi amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli na viongozi mbalimbali walioshiriki msiba wa mumewe aliyefariki dunia Mei 2, 2019.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 19, 2019 katika hafla ya kuwatambulisha mabalozi 10 wa tuzo za mafanikio kwa watu wenye ulemavu za I Can 2019.

Jackline ambaye ni mdhamini wa taasisi ya Reginald Mengi PWD, amesema baada ya mumewe kufariki dunia anachopaswa kufanya ni kutoa shukrani kwa jamii.

"Natoa shukrani kwa Rais John Magufuli, makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge na viongozi wote wa kisiasa, kidini, vyombo vya dola, vyama vya siasa, sekta binafsi na wananchi wote kwa kuonyesha mapenzi ya dhati kwa mume wangu katika safari yake ya mwisho," amesema.

Amesema heshima aliyopewa Mengi imetafsiri alichokitoa kwa jamii, familia yake itaendeleza alipoishia.

“Mimi ni mjane naamini Mengi ameacha alama kubwa na funzo kwa jamii kuhusu kutambua na kuheshimu watu wenye ulemavu na hiyo ndiyo heshima ya pekee itakayodumu kwa miaka mingi.”

“Wakati wa uhai wake alitumia uwezo na ushawishi wake katika kutetea, kuwawezesha kiuchumi, afya, michezo na kuchangamana nao kupitia hafla ya chakula cha pamoja," amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Shimimana Ntuyabaliwe amesema mabalozi hao wametokana na washindi wa tuzo za mafanikio za I can.

Amesema mabalozi hao watatumika kukuza na kuendeleza urithi wa Mengi kupitia taasisi hiyo kwa kuijenga na kuitangaza.

Moja wa mabalozi hao ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu huria, Dk Khadija Gilala amesema, "Tutakuwa mabalozi wazuri na tutasimama kwa nafasi yake kuhakikisha tunabadili mtazamo hasi juu ya watu wenye ulemavu."