Jalada kesi ya Maimu, wenzake kurudishwa kwa DPP

Muktasari:

Kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019, iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayowakabili Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano imeshindwa kuendelea kutokana na jalada la kesi hiyo kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ( DPP).

 Dar es Salaam. Jalada la  kesi ya  kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh1.175 bilioni, inayomkabili  aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP) kwa ajili ya kulipitia.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 100, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019, iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo, leo Jumanne Juni 25 2019, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai  mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally  kuwa, jalada la  kesi hiyo limerudishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kukamilisha upelelezi.

" Hivyo, kutokana na hali hii tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" alidai Swai.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemruhusu mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo, Sabina Raymond kusafiri nje ya mkoa wa Dar Es Salaam.

Hatua hiyo inatokana na mshtakiwa huyo kuwasilisha ombi hilo mahakamani hapo kupitia wakili wake Queen Allen, akiomba ruhusa ya kwenda mkoani Morogoro kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.

" Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa wa sita katika kesi hii anaomba ruhusa ya kusafiri kwenda Morogoro, ana matatizo ya kifamilia, lakini siku kesi hii itakapotajwa atakuwepo mahakamani hapa" amedia  Allen.

Allen baada ya kueleza hayo, upande wa mashtaka umedai hauna  pingamizi juu ya ruhusa hiyo kutokana na mshtakiwa huyo kuwa nje kwa dhamana.

Hakimu Ali, baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema maombi ya mshtakiwa wa sita yamekubaliwa na Mahakama.

" Mahakama imekuruhusu wewe mshtakiwa wa sita kusafiri kwenda mkoani Morogoro, lakini kesi hii itakapotajwa unatakiwa uwepo mahakamani hapa" amesema Hakimu Ali .

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ali  ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 8, mwaka 2019 itakapotajwa.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Meneja Biashara wa (Nida), Aveln Momburi; Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege; Ofisa Usafirishaji, George Ntalima; Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Hata hivyo, katika mashtaka hayo, mshtakiwa Momburi na Raymond wao hawana mashtaka ya utakatishaji, hivyo wako nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana yao Mahakama Kuu.

Kati ya mashtaka hayo 100 yanayowakabili washtakiwa hao;  mashtaka 24 ni ya kutakatisha fedha,  23 ya kughushi, 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la  kumdanya mwajiri, mashtaka matano ni ya  kuisababishia hasara Mamlaka hiyo.

Pia, mashtaka mawili ya kula njama ya kulaghai, mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka lipo moja ambalo linamkabili  Maimu na Sabina.