Japan yaimwagia mamilioni Tanzania

Muktasari:

  • Ubalozi wa Japan umetoa msaada kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za afya, maji na elimu. Jumla ya Sh615 milioni zimetolewa kwa ajili ya miradi hiyo katika mikoa ya Kusini Pemba, Mjini Magharibi na Rukwa.

Dar es Salaam. Serikali ya Japan imetoa msaada wa Sh615 milioni kwa ajili miradi mitatu ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya inayotekelezwa katika mikoa ya Rukwa, Kusini Pemba na Mjini Magharibi, Zanzibar.

Mkoa wa Kusini Pemba utapokea Sh288 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari ya Juma Pindua, mkoa wa Mjini Magharibi utapokea Sh188 milioni kwa ajili ya usambazaji wa maji na mkoa wa Rukwa utapokea Sh139 milioni kwa ajili ya kufunga vifaa kwenye vyumba vya upasuaji katika hospitali za Kirando na Mwimbi.

Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo leo Jumatatu Februari 18, 2019 Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto amesema walibaini kwamba kuna changamoto katika maeneo mbalimbali, hivyo wameamua kusaidia wananchi kupata huduma za afya na maji na wanafunzi kupata mabweni.

"Serikali ya Japan ingependa kuendelea kutoa misaada yake ya mahitaji muhimu kwa binadamu nchini Tanzania kupitia mfuko wake wa misaada. Nina matumaini kuwa utiaji saini wa mradi huu leo ni hatua nyingine kubwa inayoimarisha mahusiano yetu mazuri," amesema Balozi Goto.

Mikataba hiyo imesainiwa kati ya ubalozi wa Japan na Taasisi ya Benjamin Mkapa, Taasisi ya Maendeleo na kupunguza umasikini (Dipa), halmashauri ya wilaya ya mkoani iliyopo Zanzibar.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro amesema ni mara ya pili taasisi hiyo inapokea msaada kutoka ubalozi wa Japan kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na watoto.

"Taasisi ya Benjamin Mkapa imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali nchini, wilaya tatu za mkoa wa Rukwa zimenufaika na miradi hiyo ambayo imejikita katika kuboresha afya ya uzazi na huduma kwenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi," amesema mtendaji huyo.