Jiko la mkaa lasababisha vifo vya watoto wawili Tarime

Muktasari:

 

  • Watoto wawili wa familia moja wilayani Tarime mkoani Mara, wamefariki dunia baada ya kukosa hewa sababu ikiwa ni jiko la mkaa lililokuwa katika chumba chao cha kulala.

Tarime. Jiko la mkaa lililokuwa ndani limesababnisha vifo vya watoto wawili baada ya kukosa hewa wakati wakiwa wamelala usiku.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 3, 2019, katika mtaa wa Kebaga, wilayani Tarime mkoani Mara kwa watoto hao Witness Machugu (1) na Christina Marwa mwenye umri kati ya miaka 12-13 wakiwa wamelala chumba kilichokuwa na jiko la mkaa huku madirisha yakiwa yamefungwa.

Babu wa marehemu hao, Hobo Kihugi alisema mkwe wake aliweka jiko hilo kwenye chumba cha watoto jana usiku kwa lengo la kuandaa uji wa watoto.

Kamanda wa Polisi, Tarime-Rorya hajazungumzia tukio hili licha ya gari la polisi na askari kufika nyumbani kwa marehemu kuuchukua mwili wa Witness na kuupeleka chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mji wa Tarime.

Mwili wa Christina ulibaki nyumbani kwa ndugu zake wakidai wanataka kuuzika kwani taratibu zote zilikuwa zimekamilika ikiwamo kuchimba kaburi. Hata hivyo, polisi wamedai haiwezekani kwani lazima uchunguzi ufanyike.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachojiri