Jokate ampongeza ‘Konki Liquid’

Monday April 01 2019
pic jokate

Peter Molel maarufu Konki Liquid 'Pierre'

Dar es Salaam. Sakata la Peter Molel maarufu Konki Liquid 'Pierre' limechukua sura mpya baada ya watu mbalimbali mashuhuri kumkingia kifua, akiwemo mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzungumza katika halfa ya Tokomeza Zero Kisarawe, akivitaka vyombo vya habari kuwaibua watu wanaofanya mambo ya maana huku akimtolea mfano Konki Liquid kuwa ni mtu wa ajabu aliyepewa umaarufu bila sababu.

"Nimefurahi sana kumuona mama aliyepita hapa mbele kwa kweli ni mama wa mfano, na ningewasihi sana waandishi wa habari akina mama kama hawa wanaohangaika kwa ajili ya elimu za watoto wao ndiyo wapewe kipaumbele siyo hao walevi walevi hao akina Pierre sijui akina nani, yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndiyo wanakuwa maarufu halafu watu wa maana hawajulikani walipo," alisema Makonda.

"Hauwezi kuwa na taifa linapromote watu wa hovyo wanakuwa mpaka mabalozi unategemea watoto wetu watafika kwenye mafanikio kweli, mwingine alipitapita hapa Dk Shika yule sijui kaishia wapi nadhani watu kama hawa wanapaswa kupewa sapoti siyo hao walevi mnaotutangazia." 

Kauli hiyo imeibua mjadala  mitandaoni na leo Jumapili Machi 31, 2019 muandaaji wa shughuli hiyo Jokate ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kushukuru watu mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo akiwemo Konki Liquid.

“Hakuna maneno muhimu na machache katika ustawi wa maisha ya binadamu kama tafadhali, asante na samahani. Katika dhifa niliyoiandaa jana, nilialika watu wengi, wanasiasa, taasisi za kiserikali, mabalozi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wasanii, wadau wa burudani n.k,” amesema.

Advertisement

 “Na kwangu mimi na wilaya nzima ya Kisarawe wote waliofika jana ni muhimu sana sana kwangu na kwetu.”

Katika kuonyesha sababu iliyomfanya kiongozi huyo kuandika ujumbe huo, amesema kipekee anamshukuru Konki Liquid @officialpiere_liquid kwani wapo watu maarufu aliowaalika lakini hawakuweza kufika.

“Ila wewe ulichukua muda wako kuhamamisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa Sh100,000! Hukuja kuuza sura tu! Nasema asante sana. Wana Kisarawe tunakupenda na tunakukaribisha kuwekeza Kisarawe uanzishe hata mgahawa tutakusaidia kupata eneo.

“Lakini pia nimesikia ni mtengenezaji mzuri sana wa furniture. Hii shule tunayoenda kujenga inahitaji madawati naomba tufanye kazi na wewe katika hii fursa. Tuangalie namna japo kidogo tukuwezeshe. 

Tunasema karibu Kisarawe ukae. Kisarawe Kunogile. Tunasema samahani kwa kukwazika lakini zaidi Asante kwa kushiriki kwenye #TokomezaZeroKisarawe #ElimuItabakiKuwaJuuKileleni #KisaraweMpya Ubarikiwe!” Aliandika.

Wakati huohuo, msanii Zuwena Mohamed maarufu Shilole ameandika ujumbe akiomba msamaha kwa Watanzania kutokana na lile alilolizungumza jana.

“Kwanza, nikiri kwamba nimeona wengi niliowakwaza kutokana na maneno niliyoongea jana kwenye tukio lilioandaliwa na rafiki yetu Jokate Mwegelo. Kwa kuwakwaza huko bila hata kwenda mbali kutoa maelezo yoyote, naomba radhi, mnisamehe sana.”

“Pili, nahisi kuna namna sijaeleweka au mimi sikuweka vizuri maelezo yangu. Hoja yangu ilikuwa "Kuna vitu vya msingi hamzungumzi ila vitu vya ajabu mnazungumza....." ukisikiliza ile video utasikia mstari huo. Hicho ndio kitu nilichotaka kueleza, sio kumkashifu Pierre au mtu mwingine yeyote. Iwapo Pierre ni mmoja kati ya watu waliokwazika, namuomba sana anisamehe.” Aliandika.

Shilole alisema kufuatia hilo watu wengi wameamua kurudi nyuma na kwenda kutafuta matukio yake ya nyuma alitokea wapi mpaka kufika alipo.

“Niwahakikishie kwamba mimi nafahamu upendo mkubwa wa Watanzania kwangu kiasi kwamba walinibeba hata pale nilipokosea, walinivumilia katika ujinga wangu na bado wanaendelea kunivumilia, wananipenda licha ya uelewa wangu mdogo na walinipa nafasi kujifunza, kujirekebisha na kukua hadi hapa nilipo,” aliandika Shilole na kumalizia hashtag #ChiiiiiiiiiiiiWatanzaniaMtabakiKuwaJuuuu

 

Advertisement