Joshua Nassari apoteza sifa ya kuwa mbunge

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari

Muktasari:

  • Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge baada ya kushindwa kuhudhuria vikao vya mikutano mitatu ya Bunge la Tanzania

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Machi 14, 2019 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge, imeeleza jimbo hilo linaloongozwa Joshua Nassari (Chadema) lipo wazi kutokana na mbunge huyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.

“Mheshimiwa Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kitendo chake cha kutohudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Mikutano hiyo ni ule wa 12 wa Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na mkutano wa 14 wa 29 Januari hadi Februari 9 mwaka 2019.

Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1)(c)  inayoeleza kuwa “Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.”

Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika Kanuni ya 146 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo ya Januari 2016.

Kanuni hiyo inaeleza “kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”

Kufuatia barua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki.