Kagame bingwa Afrika kufanikisha afya kwa wote

Tuesday March 5 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Kigali, Rwanda. Rais wa Rwanda, Paul Kagame ametajwa kuwa kiongozi mahiri Afrika kwa kufanikisha upatikanaji huduma za afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi, (UHC) baada ya asilimia 90 ya wananchi wake kuwa na bima za afya.

Kagame amekabidhiwa tuzo hiyo leo Jumanne Machi 5, 2019 katika mkutano uliozikutanisha nchi zote Afrika kujadili masuala ya afya 'Africa Health 2019', huku Tanzania ikikosa uwakilishi.

Katika mkutano huo ajenda kuu inazungumzia uboreshaji huduma za afya kwa wote, ikiwa ni utekelezaji wa lengo namba tatu la mpango wa maendeleo endelevu.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk Diane Gashumba amesema mafanikio hayo yamewezekana baada ya nchi hiyo kuwekeza katika afya ya msingi, ikiwemo watoa huduma ngazi ya jamii ambao walisaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima za afya.

“Rwanda imefanikiwa kuwafikia asilimia 90 ya wananchi wake katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo Endelevu ulioanzishwa mwaka 2015 unaotarajiwa kumalizika mwaka 2020, tunatarajia kuwafikia wote ifikapo 2021,” amesema Dk Gashumba.

Akizungumza awali, mtoa huduma ngazi ya jamii, Beatrice Nyindebera amesema, “awali kabla ya kuwa na watoa huduma ngazi ya jamii, wengi hawakujua umuhimu wa huduma za afya na tumefanikiwa katika kuelimisha wananchi wengi kujiunga na bima za afya.”

Naye Waziri wa Afya wa Uganda, Sarah Opendi amesema ingawa bado hawajafikia malengo katika bima za afya kwa wote, watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa msaada mkubwa katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

“Serikali inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na tunatarajia ifikapo 2021 tutakuwa tumefikia hatua nzuri katika huduma za afya kwa wote.”

Mawaziri na manaibu waziri wa afya kutoka nchi mbalimbali leo wanaendelea kujadiliana kuhusu ajenda hiyo na namna ambavyo wataifikia, huku Tanzania ikikosa uwakilishi.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Tanzania ipo katika mchakato wa kupeleka muswada wa huduma za afya kwa wote bungeni ifikapo Aprili mwaka huu, ili kutungiwa sheria.

Endelea  kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri kwenye mkutano huo


Advertisement