Kakobe awazulia jambo Chadema, awataka watubu hadharani

Askofu Mkuu wa Kanisa la FGBF, Zachary Kakobe akihutubia wakati wa ibada ya jumapili katika kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe leo Jumapili ametumia ibada kuwataka viongozi Chadema waliotukana viongozi wa dini watubu vinginevyo chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu zaidi.

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema yeye na kanisa hilo si wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Pia, amewataka viongozi wa Chadema waliotukana viongozi wa dini watubu hadharani, wasipofanya hivyo, chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu zaidi, hawataweza kuinuka tena.

Kiongozi huyo wa FGBF ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 27, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa ibada kufuatia siku za hivi karibuni kuonekana mara kadhaa kwenye hafla za Rais John Magufuli na kupewa nafasi ya kuomba.

Hata hivyo, amesema aliwahi kuhudhuria mkutano mmoja tu wa Chadema uliofanyika Mlimani City na kwamba katika mkutano huo alihudhuria si kama mwanachama bali kama baba ambaye anaweza kualikwa na watoto wengi.

"Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, sijawahi kuwa na mazungumzo naye; iwe kanisani au nyumbani au mahali popote. Hata katika mkutano ule nilipokelewa na viongozi wengine kabisa," amesema Askofu Kakobe.

Amesema hajawahi kuonana wala kuzungumza kwa simu na mbunge wa jimbo la Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ambaye anaongoza eneo ambalo kanisa lake lipo.

"Kama hamjui, nimehudhuria mikutano mingi zaidi ya CCM kuliko Chadema. Nakumbuka wakati mmoja niliwahi kuhudhuria mkutano wa wazee kumuaga Rais Benjamin Mkapa, nilialikwa na Yusuph Makamba. Wakati ule nilihudhuria mikutano mingi kwa sababu Makamba ni rafiki yangu sana," amesema.

Askofu Kakobe amesema kuhudhuria kwake mikutano ya Rais Magufuli kumeibua mitazamo tofauti, wengine wakisema ameahidiwa ubunge na wengine wakisema amenunuliwa. Hata hivyo, amekanusha madai hayo.

 

"Wanasema 'sasa inakuwaje umeanza kuandamana na Rais Magufuli, umeahidiwa ubunge? Nianze kukaa bungeni miezi mitatu, nani atafanya kazi hii. Hata nikiteuliwa, nitasema asante, nimeitwa kwa kazi moja tu."

"Wengine wanasema labda amenunuliwa, mimi? Si mnaelewa nina hela? Si wanafahamu nilisema nina hela kuliko Serikali? Si wanafahamu TRA walikuta fedha nzuri tu kwenye akaunti ya kanisa? Sasa unaninunua kwa bei gani, sina bei," amesema Askofu Kakobe huku waumini wake wakimshangilia.