Kamati kuu Chadema leo, Mbowe, Sumaye hawapo

Dar es Salaam. Wakati kamati kuu ya Chadema ikikutana leo bila uwapo wa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye yuko mahabusu kwa tuhuma za kukiuka masharti ya dhamana katika kesi yake ya uchochezi, mjumbe mwingine wa kikao hicho, Frederick Sumaye ameugua ghafla.

Sumaye ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu ameugua ghafla akiwa ziarani jijini Tanga kwa shughuli za kichama na kulazwa katika hospitali ya mkoa huo ya Bombo.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene jana alisema Sumaye alijisikia vibaya jana asubuhi hivyo kupatiwa huduma hospitalini hapo na jitihada za kumhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi zinafanyika. Kuhusu kikao cha kamati kuu, Makene alisema ni cha siku moja chenye ajenda kuu ya hali ya kisiasa nchini.

Licha ya kwamba taarifa hiyo kutoweka bayana ‘hali ya kisiasa’ itakayojadiliwa, kikao hicho kinafanyika wakati chama hicho kimekuwa kikilalamika kukakabiliwa na hali ngumu kisiasa inayotishia mustakabali wake.

Suala la Mbowe na mbunge mwenzake, Esther Matiko walioko mahabusu pia linaweza kuchukua nafasi kwenye kikao hicho. Wabunge hao wako mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili sasa huku hatma yao ikiwa haijulikani.

Vilevile kupitishwa bungeni kwa sheria ya vyama vya siasa hivi karibuni huenda pia ni suala litakalochukua nafasi kutokana na kulalamikiwa kwa madai ina vifungu vingi vinavyowabana na ambavyo wanadai vinaielekeza nchi kurudi katika mfumo wa chama kimoja na hatima ya mbunge wake, Tundu Lissu ambaye anayefanya ziara katika nchi za Ulaya na Marekani kufafanua jaribio la mauaji ambalo pia linahatarisha ubunge wake huenda nalo likawa agenda ya kikao hicho.