Serikali yasitisha mikutano ya hadhara vyama vya siasa Tanzania
Muktasari:
- Kauli hiyo imetolewa leo Juni 26, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Paschal Chinyele.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imetangaza kusitisha mikutano ya hadhara kwa vyama vyote nchini kwa sababu ya kile ilichoeleza kuwa ni kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki kuelekeza Maonyesho ya Biashara ya Sabasaba.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 26, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Paschal Chinyele.
Chinyele alitaka kufahamu kama Serikali inafahamu kuhusu kuwepo kwa tetesi za maandamano zinazosababisha taharuki kwa wananchi.
Mbunge huyo, pia, alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuwahakikishia Watanzania usalama wao na mali zao.
Spika wa Bunge, Mussa Zungu alimsimamisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Katambi akimtaka kujibu mwongozo huo.
Akijibu mwongozo huo, Katambi amesema ni kweli kuna taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikisema kutakuwa na maandamano, japo hakuna sababu zinazotajwa kwenye taarifa hizo.
Amesema wapo wanaosema kutakuwa na maandamano lakini sababu hazitajwi, hata wale waliojaribu kutaja sababu, ni zile ambazo Serikali imezitolea suluhisho moja wapo likiwa la Katiba mpya, ipo kwenye ilani ya CCM na hatua mbalimbali zimepangwa za kiserikali katika namna ya kuliendea jambo hilo
Katambi amesema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama na tayari wameanza kufuatilia viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, kwa yeyote anayepanga kuvuruga amani kupitia mitandao ya kijamii au moja kwa moja.
“Namuagiza IGP Camilius Wambura, atoe maelekezo kwa ma-RPC wote nchini, ambayo yatashuka kwa wakuu wa Polisi Wilaya mpaka kwenye Polisi Kata kuanza kufanya uratibu wa mipango ya kiusalama na kuiimarisha zaidi,” amesema.
Amesema hivi karibuni Tanzania inatarajia kuwa na ugeni katika Maonyesho ya Sabasaba ambapo inatarajia kupata wageni kutoka mataifa mbalimbali. Amesema kipindi hicho ndiyo kinasaidia kujijumuisha katika kujenga uchumi wa nchi.
Waziri huyo ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho kuna chokochoko hizi, hawataweza kumvumilia mtu yeyote ambaye atafanya vurugu za aina yoyote kwani ni kipindi ambacho wanatarajia shughuli zote za kiuchumi ziendelee.
“Namuelekeza IGP Wambura asitoe vibali kwa kazi zozote zitakazokuwa zinahusiana na kufanya mikutano ya hadhara katika kipindi hiki, kwa chama chochote, iwe Chama cha Mapinduzi, iwe chama chochote kile, kwa kipindi hiki.
“Ni vizuri tukarudi katika kuruhusu wananchi kujenga uchumi wa nchi yao. Ni katika kipindi ambacho tunahitaji kufanya kazi kuhakikisha kila Mtanzania, wafanyabiashara, wawekezaji wanafanya kazi zao kwa utulivu,” amesema.
Katambi amesema kuanzia kesho wataanza kuwahoji watu tofauti ambao wamekuwa waziwazi, kwa ushahidi na vielelezo, wakichochea uvunjaji wa amani katika taifa hili, kufanya vurugu na wanazo clip za video ambazo wamezungumza kwenye majukwaa mbalimbali.
Licha ya zuio hilo la mikutano ya hadhara lililowekwa na Serikali, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kama haki ya kisiasa.
Awali, kuhusu tetesi za maandamo ya Sabasaba, wiki kadhaa kumekuwepo na taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa huenda kukawepo maandamano yasiyo na kikomo ambayo waratibu wake hawajulikani, yakilenga kuhusu madai ya Katiba Mpya na Free Tundu Lissu.