Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kihongosi aeleza umuhimu wa ziara zake

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi akizungumza wakati wa ukaguzi mradi wa umwagiliaji Mgambalenga Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo. Picha na CCM

Muktasari:

  • Asema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi.

Kilolo. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amesema chama hicho kitaendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo nchini ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Amesema ufuatiliaji huo ni sehemu ya majukumu ya chama katika kuhakikisha ahadi zinazotolewa na Serikali zinatekelezwa kwa vitendo katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza Juni 19, 2026 katika ziara yake wilayani Kilolo, Kihongosi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakilalamikia ziara za ufuatiliaji wa miradi, lakini ziara hizo ni muhimu kwa sababu zinatoa fursa ya kujionea maendeleo yanayoendelea na changamoto zilizopo ili zitatuliwe kwa wakati.

“Tumewaahidi wananchi tutajenga vituo vya afya, tunazunguka mtuonyeshe kituo cha afya mlichojenga kiko wapi?” amesema Kihongosi na kuongeza kuwa:

“Tukiona mmejenga hapo sawa, lazima tuwe chama cha kusimamia misingi kwani bila CCM madhubuti nchi itayumba,” amesema.

Kihongosi amehoji namna wananchi wanavyoweza kuona matokeo ya miradi kama vile vituo vya afya na miundombinu mingine bila kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali.

“Na niseme tu lengo la ziara hizi si kuingilia kazi za watendaji wa Serikali, bali ni kuhakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia matarajio ya wananchi,” amesema Kihongosi.

Aidha, amewataka wananchi na viongozi kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi, akisema amani ni msingi muhimu wa maendeleo.

“Kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani na kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na mambo yanayoweza kuvuruga utulivu wa nchi,” amesema Kihongosi.

Kwa upande wake, viongozi wa CCM wa Wilaya ya Kilolo wamesema wataendelea kushirikiana na wananchi pamoja na Serikali katika kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Awali, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Juni 18, 2026 katika Uwanja wa Sokoni, Kata ya Ruaha Mbuyuni, mkoani Iringa, Kihongosi alisema ziara za viongozi zina umuhimu wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.

Kihongosi alimweleza Waziri Aweso kuhusu changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Ruaha Mbuyuni, huku akieleza kuwa wananchi wanahitaji hatua za haraka.

Waziri Aweso aliunganishwa moja kwa moja kwenye kipaza sauti, hatua iliyosababisha shangwe kwa wananchi.

Akijibu mbele ya umati huo, Waziri Aweso alisema Serikali imejipanga kumaliza kero ya maji katika eneo hilo.

“Naomba niwahakikishie wananchi wa Ruaha Mbuyuni kwamba Serikali imeweka kipaumbele kikubwa kwenye maji na natoa ahadi ya Sh500 milioni kukamilisha mradi huu ili kuhakikisha mnapata maji safi na salama,” alisema Aweso.

Baada ya mawasiliano hayo, Kihongosi alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na huduma muhimu.

“Tunachokifanya hapa ni kusikiliza wananchi na kuhakikisha kila changamoto inafikishwa kwa wahusika na kutatuliwa kwa wakati, na hii ndiyo dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema.

Mbunge wa Kilolo, Ritta Kabati alisema ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa vizuri na kuleta tija kwa jamii.

Wananchi waliozungumza katika mkutano huo waliipongeza Serikali kwa kusikiliza kero zao kwa kuwa maji ni muhimu katika maisha ya kila siku.

“Hatukuwahi kufikiria kama tunaweza kusikilizwa moja kwa moja hivi na leo tunaona matumaini mapya ya kupata maji baada ya muda mrefu wa mateso,” alisema Michael Mofuga, mkazi wa Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo.

Naye mkazi mwingine, Baraka Mollel, alisema mradi huo ukikamilika utaondoa kabisa adha ya wanawake kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuboresha maisha ya jamii kwa ujumla.

Mkutano huo uliendelea kwa maswali na majibu ya wananchi huku viongozi wakiahidi kushughulikia changamoto nyingine za kijamii na kiuchumi zilizotajwa.