Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili walivyochuana mahakamani kesi ya ubunge wa Baba Levo

Muktasari:

  • Kesi hiyo imefunguliwa na Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kigoma Mjini, mbunge wa jimbo hilo, Clayton Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)



Kigoma.  Wakili wa walalamikaji katika kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, John Seka ameieleza Mahakama kuwa, walalamikaji wameshindwa kuwasilisha kwa wakati maelezo ya mashahidi wao kutokana na kupewa muda mfupi.

Wakili Seka amebainisha hayo leo Juni 18, 2026, wakati wa usikilizwaji wa maombi madogo ya nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo hayo yaliyowasilishwa na walalamikaji hao.

Hata hivyo, hoja za walamikaji hao zimepingwa na mawakili wa utetezi, Daniel Rumenyela na Thomas Msasa wakidai walalamikaji wamefanya uzembe na kupuuza amri ya Mahakama na kwamba, kiapo kinachounga mkono maombi hayo kinasoro za kisheria zisizotibika.

Kesi hiyo imefunguliwa na  Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kigoma Mjini, mbunge wa jimbo hilo, Clayton Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanapinga ubunge wa Baba Levo (CCM), aliyetangazwa kushinda kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimzidi mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.

Wanadai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro za ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi pamoja na vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Baada ya kukamilika kwa usikilizwaji wa awali wa kesi, Juni 15, 2026, Mahakama ilipanga kuanza usikilizaji wa kesi hiyo katika hatua ya ushahidi wa walalamikaji kuanzia leo Juni 18, 2026 saa 6:00.

Pia, iliwaamuru walalamikaji kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi wao, ndani ya siku 18 kabla ya muda uliopangwa wa kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo, kwa mujibu wa kanuni ya 21(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Wabunge na Rais za Mwaka 2025.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo usikilizwaji wa mashauri ya ubunge utafanyika kwa njia ya maelezo ya maandishi ya mashahidi.

Kanuni ya 21(3), inamtaka mlalamikaji kuwasilisha kwa msajili maelezo ya kila shahidi yakieleza kiini cha ushahidi wake ndani ya saa 48 baada ya usikilizwaji wa awali kukamilika kabla ya muda uliopangwa kuanza usikilizwaji.

Hata hivyo, walalamikaji hawakuweza kuwasilisha maeleezo hayo ndani ya muda, hivyo Juni 17, walifungua maombi madogo wakiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wa walalamikaji hao, Seka ameieleza Mahakama kuwa, walalamikaji wameshindwa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi kutokana na ufinyu wa muda waliopewa.

Amedai uamuzi wa Mahakama kutoa muda huo kwa walalamikaji ulitokana na tafsiri ya Mahakama ya kanuni hizo.

Akichanganua muda huo, wakili Seka amesema kwa mujibu wa amri ya Mahakama kulingana na kanuni hizo, maelezo hayo yalipaswa kuwasilishwa kwa msajili kabla ya saa sita mchana, Juni 16, 2026.

Amesema kwa kuwa usikilizwaji wa awali ulichelewa kukamilika ambao uliisha saa 12 basi kutoka Juni 15, 2026 saa 12 mpaka Juni 16 kabla ya saa sita mchana ni saa 18 tu.

Amedai ndani ya saa hizo 18 kuna saa 12 zisizo za kazi yaani usiku, hivyo walalamikaji walikuwa na saa sita tu za kutekeleza amri hiyo, yaani kuwatafuta mashahidi 20, kuwahoji kuandaa nyaraka zikiwamo za kurasa 180 na za kielektroniki yaani picha jongefu (video) zaidi ya 60.

Amesema kwa mazingira hayo, jambo hilo halikuwezekana na ndio maana wanaomba kuongezewa muda kwa kuwa saa hizo sita za kazi hazikutosheleza kukamilisha jukumu hilo zito kuwasilisha ushahidi usio na shaka ili waweze kupata haki ya kusikilizwa.

Amedai walalamikaji wameweza kukidhi vigezo vya kisheria vilivyokwishawekwa na Mahakama katika uamuzi wa mashauri mbalimbali ambavyo ni pamoja na kuonesha sababu za kuchelewa, kutokuchelewa kwa muda mrefu na kwamba hawakuzembea kutafuta haki yao hiyo.

Amefafanua maombi hayo yaliyowasilishwa Juni 17, 2026 saa sita mchana, hivyo waombaji wamechelewa kwa siku moja waliyoitumia kuandaa maombi hayo na kwamba hiyo inaonesha kuwa hapakuwa na uzembe maombi hayo.


Maelezo ya Serikali

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Mark Mulwambo amesema baada ya kusoma kanuni ya 26(1), 34(2) za kanuni hizo hawana pingamizi kuwa Mahakama inaweza kuamua kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya msingi ili haki iweze kutendeka.

Ameongeza kanuni hizo zikisomwa pamoja na kifungu cha 103 na 105 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Mahakama hiyo imepewa mamlaka kutumia mamlaka yake ya asili kuongeza au kukataa kuongeza muda ili haki iweze kutendeka.

Hata hivyo, amesema Mahakama inapaswa ijiridhishe na kupima uzito wa sababu zinazotolewa za kuchelewa huko kama ni za msingi, kama ambavyo imesisitizwa na Mahakama katika uamuzi wa mashauri mbalimbali.


Wakili wa Baba Levo

Kwa upande wa mawakili wa Baba Levo, Rumenyela, ameieleza Mahakama kuwa, wakili wa walalamikaji hajasema kuwa wanaomba nyongeza ya muda kuwasilisha ushahidi wa maandishi kwenye shauri gani.

Amedai kama alikuwa anazungumzia shauri hilo la maombi madogo, hakuna amri ya Mahakama iliyotolewa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza.

Ameongeza ingawa wakili katika hoja zake ametaja kesi ya uchaguzi lakini ameitaja baada ya wao kuhoji hilo katika kiapo chao kinzani kujibu kiapo kinachounga mkono maombi hayo madogo.

Amesema hata hivyo wakati tarehe ya usikilizwaji wa kesi ya uchaguzi, wakati inapangwa tarehe hiyo ya usikilizwaji alikuwepo na alikubaliana nayo.

Hivyo, wakili Rumenyela amedai wakili wa waombaji ameonesha uzembe na dharau kwa Mahakama kwa kutokuwasilisha hata maelezo ya shahidi mmoja na hata walalamikaji wenyewe ambao wanapatikana.

Amedai kwa mujibu wa kanuni ya 21(5) wakili wa walalamikaji alipaswa kuwasilisha maelezo ya mashahidi walioweza kupatikana na wale ambao wasingepatikana basi angekuja kuieleza Mahakama na akaomba watoe ushahidi wao kwa mdomo na si kufungua maombi ya nyongeza ya muda.

Amesema saa 48 zinahesabiwa baada tu ya kukamilisha usikilizwaji wa awali na kwamba muda huo ulikuwa unaisha Juni 17, 2026 saa 12 jioni.

Vilevile amedai kuwa, walalamikaji katika maombi yao hawajaambatanisha amri ya Mahakama inayolalamikiwa na kwamba,  vifungu vya 26 na 34 vilivyotumika kufungua maombi hayo havizungumzii suala la kuongeza muda bali mamlaka ya Mahakama kuahirisha usikilizwaji shauri.

Ameongeza walalamikaji si tu kuwa wamekiuka kanuni bali pia Sheria ya Ukomo wa Muda kifungu cha 46 kwa kuwa tayari amri ya Mahakama ilishatoka na hivyo ni sheria.

Pia, amesema kiapo kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro kutokana na kutaja muda wa kukithibitisha ambao haupo kwani muda uliotajwa Desemba 24, 2025 ulishapita.

Akihitimisha hoja zake wakili Rumenyela amesisitiza walalamikaji walipewa muda wa kutosha wa saa 48 lakini hawakutaka kuzitumia kwa hasara yao wenyewe, hivyo akaiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo.

Kwa upande wake Msasa, wakili mwingine wa Baba Levo amedai kutokana na kasoro hiyo ya muda wa kuthibitishwa kiapo hicho, kinakuwa batili na kwamba kwa maana hiyo maombi hayo hayawezi kusimama.

Amedai kuwa kasoro hiyo haiwezi kurekebishika katika hatua hiyo bali marekebisho yalipaswa yaombwe kabla ya kuanza usikilizwaji.

Vilevile wakili Msasa amedai kuwa katika maombi ya kuongezewa muda lazima sababu ziorodheshwe kwenye kiapo cha kuunga mkono maombi hayo lakini sababu zilizotolewa mahakamani hazipo kwenye kiapo hicho.

Wakili Msasa amedai kuwa, amri ya Mahakama licha ya kwamba haijaambatanishwa lakini hakuna mahali ambapo ilielekeza kuwa wakili wa walalamikaji anatakiwa kuwaita na kuwahoji mashahidi wake wote bali alitakiwa kuwasilisha mahakamani maelezo yao.

Wakili Seka akijibu hoja za mawakili hao amefafanua kuwa, maombi yaliyoko mahakamani ni kuongezewa muda na si kupinga amri ya Mahakama na kwamba hawapingi amri ya Mahakama ambayo imefuata misingi ya kanuni ndiyo maana hawakuiambatanisha.

Amedai hoja yao ni kwamba wao ndiyo wameshindwa kukidhi matakwa ya kisheria na amri ya Mahakama kwa kuwa, kwa tafsiri yao walipewa muda mfinyu wa saa 18 zikiwamo saa 12 zisizo za kazi, hivyo kubakiwa na saa sita tu za kutekeleza amri hiyo ya Mahakama.

Amedai maombi ya kuongezewa muda hayana ukomo wa kisheria na kwamba katika kuomba kuongezewa muda wametumia kifungu cha 103 cha Sheria ya anCPC, ambacho kinaruhusu kuwasilisha maombi hayo ndani au nje ya muda uliopangwa na Mahakama na cha msingi ni kueleza sababu.

Amefafanua kuwa maombi hayo kama kichwa cha habari kinavyojieleza ni ya nyongeza ya muda kwenye shauri la msingi ambalo limetajwa (kesi ya uchaguzi) na kwamba hakuna mahali walikokosea.

Kuhusu hoja ya kasoro ya kiapo, wakili Seka ameeleza kuwa, wameigundua kasoro hiyo na kama maofisa wa Mahakama wao ndio wameieleza na kubainisha kuwa kasoro hiyo inatibika.

Wakili Seka amesema kuwa hawakuweza kuwasilisha hata maelezo ya shahidi mmoja kwa kuwa waligundua kuwa wako nje ya muda ndiyo maana wakawasilisha maombi hayo mapema.

Amesema kanuni ya 21(5) inasema shahidi ambaye maelezo ya ushahidi wake hayako mahakamani hataruhusiwa kutoa ushahidi isipokuwa kwa idhini ya Mahakama baada ya kuomba na kwamba kanuni hiyo haisemi kuwa idhini hiyo inaombwa kwenye shauri la msingi.

Akihitimisha hoja zake, wakili Seka amesisitiza kuwa wameonesha sababu za kutosha kuongezewa muda ili waombaji wapate haki ya kikatiba kusikilizwa kikamilifu na kwamba kasoro zilizojitokeza zikiwamo za kikanuni zinatibika.

Jaji Victoria Nongwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo kwa saa moja kwa ajili ya kuandaa uamuzi.