Prime
Mapya katikati ya usikilizwaji wa kesi ya ubunge wa Baba Levo
Muktasari:
- Kesi ya uchaguzi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Kigoma Mjini mwaka 2025, ambapo mgombea wa CCM alitangazwa mshindi, sasa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi baada ya taratibu za awali kukamilika.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, imepanga kuanza kusikiliza kesi ya uchaguzi wa jimbo la Kigoma Mjini leo, Alhamisi, Juni 18, 2026, kuanzia saa 6:00 mchana katika hatua ya ushahidi.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa taratibu za awali na za msingi za usikilizaji wa kesi hiyo, ambazo zimehitimishwa kupitia hatua ya usikilizwaji wa awali iliyofanyika Jumatatu, Juni 15, 2026, jioni.
Hata hivyo, kabla ya Mahakama kuanza kusikiliza ushahidi wa walalamikaji, kwanza itasikiliza shauri dogo la maombi ya nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo ya maandishi ya mashahidi wa walalamikaji.
Wakili wa walalamikaji katika kesi hiyo, John Seka, ameliambia Mwananchi leo, Alhamisi, kuwa hadi sasa hawajawasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi na kwamba wameomba nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo hayo.
“Kwa hiyo tutaanza kwanza kusikiliza shauri dogo la extension of time (nyongeza ya muda) la kuwasilisha maelezo ya mashahidi, halafu ndipo kesi ya msingi itaanza kusikilizwa saa 6:00 mchana,” amesema Wakili Seka.
Hata hivyo, Wakili Seka amesema usikilizwaji wa kesi ya msingi utategemea sana uamuzi wa Mahakama kuhusu maombi hayo madogo ya nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi.
“Kama Mahakama haitakubali maombi haya, basi uamuzi huo unaweza kuiondoa petition (kesi ya ubunge) mahakamani,” amesema Seka.
Hii inamaanisha kuwa athari ya uamuzi wa Mahakama katika maombi hayo madogo, iwapo hayatakubaliwa, ni kwamba kesi hiyo itaondolewa mahakamani, kwani bila kuwepo kwa maelezo ya mashahidi mahakamani, mashahidi hao hawawezi kutoa ushahidi na hivyo hakutakuwa na kesi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Clayton Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo, alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo na hivyo kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Baba Levo alitangazwa kushinda kiti hicho akimzidi mpinzani wake mkubwa kutoka chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne--- Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wamefungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakipinga uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, wadai hao, ambao wanajitambulisha kuwa wapiga kura katika jimbo hilo, wanadai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.
Wanabainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, pamoja na vitendo vya rushwa na udini vinavyodaiwa kufanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba Mahakama hiyo, pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Serikali, kwa upande mmoja, na Baba Levo, kwa upande mwingine, wamekuwa wakiibua mapingamizi mbalimbali, wakiishawishi Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila kusikiliza ushahidi wa madai hayo, wakidai kuwa imegubikwa na kasoro mbalimbali za kisheria.
Jitihada za wadaiwa hao za kutaka kuimaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi kupitia mapingamizi ya awali ya hoja za kisheria zimegonga mwamba, kwani mara kadhaa Mahakama hiyo imekuwa ikiyakataa mapingamizi hayo.
Kutokana na mvutano huo, muda wa awali wa usikilizwaji wa kesi za uchaguzi uliisha hata kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kwa madai ya msingi, jambo ambalo limemlazimu Jaji Mkuu, George Masaju, kwa mamlaka aliyo nayo kisheria, kuongeza muda wa miezi sita wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Baada ya kupenya katika mapingamizi hayo, Juni 15, 2026, kesi hiyo iliingia katika hatua ya usikilizwaji wa awali, ikiwa ni maandalizi ya usikilizwaji kamili wa madai ya msingi.
Katika hatua hiyo, wadaiwa walisomewa muhtasari wa madai ya kesi hiyo na kisha wakatakiwa kubainisha mambo au hoja wanazokubaliana nazo na zile wasizokubaliana nazo katika maelezo hayo, ambazo ndizo upande wa wadai utakuwa na wajibu wa kuzithibitisha.
Wakili wa wadai, John Seka, aliiambia Mahakama hiyo kuwa wadai wanatarajia kuwaita mashahidi wasiopungua 20 na kuwasilisha vielelezo mbalimbali.
Baada ya hatua hiyo, ndipo Mahakama ikapanga kuanza kupokea ushahidi huo leo, iwapo maombi hayo madogo ya nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi yatakubaliwa.