Kihongosi aagiza mradi wa Mgambalenga ukamilike kwa wakati
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi akizungumza wakati wa ukaguzi mradi wa umwagiliaji Mgambalenga Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo. Picha na CCM
Muktasari:
- Mradi wa huo wa Umwagiliaji Mgambalenga unaotekelezwa katika Kata ya Ruaha Mbuyuni, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kwa gharama ya Sh23.9 bilioni unatarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 150 hadi 1,700.
Iringa. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa umwagiliaji wa Mgambalenga wilayani Kilolo, mkoani Iringa, kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati ili wakulima wanaotarajiwa kunufaika waweze kupata manufaa yaliyokusudiwa.
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 18, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo katika Kata ya Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo.
Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh23.9 bilioni, unalenga kuwanufaisha wakulima wa vijiji vya Mtandika, Msosa na Ruaha Mbuyuni kwa kupanua eneo la umwagiliaji kutoka hekta 150 za sasa hadi hekta 1,700.
Msafara wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi na viongozi mbalimbali wakiwa katika eneo la mradi wa Umwagiliaji Mgambalenga Ruaha mbuyuni Wilayani Kilolo. Picha na CCM
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Kihongosi amesema utekelezaji wake una umuhimu mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
“Mradi huu wa umwagiliaji wa Mgambalenga ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima. Ni muhimu ukakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huu mkubwa wa Serikali,” amesema.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Kapukutu amesema kazi hiyo inatekelezwa na kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kwa thamani ya Sh23.9 bilioni.
Mhandisi wa Umwagiliaji Wilayani Kilolo, Gerald Kapukutu akiwasilisha taarifa ya mradi ya Umwagiliaji Mgambalenga kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi na Viongozi wengine walipotembelea mradi huo kata ya ruaha mbuyuni. Picha na CCM
Amesema mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha moja kwa moja wakulima 1,129, huku wananchi wengine 38,824 wakitarajiwa kupata manufaa kupitia ongezeko la uzalishaji wa chakula, ajira na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kapukutu, kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji yenye urefu wa kilomita 44.5 kwa kiwango cha zege, vijengwa vya umwagiliaji, barabara za mashambani zenye urefu wa kilomita 31 na ofisi ya meneja wa mradi.
Amesema maandalizi ya awali ya mradi yamefikia asilimia 98, huku kilomita 4.4 za mifereji ya umwagiliaji tayari zikiwa zimejengwa kwa zege na kilomita 5.5 za barabara za mashambani zikiwa zimejengwa kwa kiwango cha changarawe.
“Hadi sasa mradi umefikia asilimia 47 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Juni 27, 2027, baada ya kuongezewa muda wa utekelezaji ili kukamilisha kazi zilizobaki,” amesema Kapukutu.
Hata hivyo, amesema mradi huo unakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo mvua nyingi zilizochelewesha baadhi ya shughuli za ujenzi, uwepo wa mazao katika maeneo yanayopitishwa mifereji ya umwagiliaji pamoja na kupanda kwa gharama za mafuta na ajira.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilolo, Ritta Kabati amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao mwaka mzima badala ya kutegemea msimu wa mvua pekee.
Naye mkulima wa Ruaha Mbuyuni, Neema Mwalukasa amesema wakulima wa eneo hilo wanausubiri kwa hamu mradi huo kukamilika kwa kuwa utaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kuongeza kipato cha kaya na kuimarisha usalama wa chakula katika vijiji vinavyonufaika na mradi huo.