Kamisheni ya Kiswahili yatoa ufadhili wa mafunzo

Muktasari:

  • Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ni asasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  iliyoanzishwa kwa itifaki iliyoridhiwa kwa pamoja na nchi wanachama wote na ilianza shughuli zake Julai 2015 ikiwa na mamlaka ya kuratibu na kuimarisha maendeleo na matumizi ya Kiswahili kwa nchi wanachama

Dar es Salaam. Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama) imedhamiria  kuwaunganisha wananchi kwenye nchi wanachama wa jumuiya hiyo ili kuleta utangamano miongoni mwao kupitia fursa ya mpango wa mafunzo maalumu iliyouanzisha.

Kamisheni hiyo yenye makao makuu mjini Zanzibar, imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele kuwaunganisha wanajumuiya lengo likiwa ni kuimairisha utangamano na kuhakikisha wananchi katika nchi wanachama wanapiga hatua za maendeleo kupitia lugha ya Kiswahili.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo, Profesa Kenneth Simala akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Aprili 5, 2019, alisema lengo la mpango huo ni kuwaunganisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuleta utangamano.

Amesema wametoa fursa ya wananchi kuomba nafasi ya mafunzo na wiki hii zoezi hilo litafungwa na kazi ya kuanza kuwachagua wenye sifa na wanaokidhi vigezo itaanza mara moja na baadaye watawasiliana na wateule kupitia anwani walizoainisha.

Profesa Simala amesema wamefurahishwa na mwitikio wa wananachi wa Jumuiya kutokana na kutuma maombi ya mafunzo hayo kwa wingi jambo ambalo limeipa faraja kamisheni.

Ameongeza kuwa mpango huo unawahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi  katika vyombo vya habari na wadau wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazofungamana na Kiswahili jambo ambalo litawaongezea ufanisi kwenye kazi zao.

Profesa Simala alifafanua kuwa mpango huo kwa sasa hautawahusu wanafunzi wa sekondari, kwa sababu itakuwa jambo gumu kuwasimamia wanapokuwa nje ya nchi zao na wengine huenda wakahitaji usimamizi wa karibu wa walimu wao.

Amesema tayari wameshazungumza na baadhi ya taasisi za vyombo vya habari kuwapokea waombaji watakaohitaji nafasi ya kwenda kujifunza na kwa hapa Tanzania wameshazungumza na wadau ambao ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Kenya wameshazungumza na KTN ili waweze kuwapokea waombaji.

Profesa Simala pia amesema kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti, kamisheni itatoa ufadhili kidogo kwa waombaji, huku akitoa rai kwa mashirika na taasisi wanakotoka waombaji iwapo watapata nafasi ya kuteuliwa, nao washiriki kuwawezesha gharama za malazi kwa kipindi chote watakapokuwa mafunzoni.

Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilianza shughuli zake Julai 2015 ikiwa na mamlaka ya kuratibu na kuimarisha maendeleo na matumizi ya Kiswahili kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.