Kampuni ya China kuwekeza Sh2.3 trilioni kuinua kilimo Tanzania

Muktasari:

Kampuni ya Super Agri Technology ya China imeingia makubaliano ya kuwekeza Dola 1 bilioni ndani ya miaka mitano nchini zitakazosaidia kuinua kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya sekta hiyo katika mwendelezo wa kuvutia wawekezaji na kuongeza tija ya kilimo.

Dar es Salaam. Baada ya mkurugenzi mkuu wa Mamlaka Ukanda wa Uwekezaji Tanzania (EPZA), Joseph Simbakalia kubainisha fursa zilizopo nchini, kampuni ya Super Agri Technology ya China imekubali kuja kuwekeza Dola 1 bilioni (zaidi ya Sh2.3 trilioni) kwenye kilimo na usindikaji mazao.

Simbakalia pamoja na maofisa wengine waandamizi wa Serikali wapo nchini China ambako pamoja na mambo mengine wamehudhuria maonyesho ya kimataifa ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika (China-Africa economic and trade expo) yanayofanyika katika Mji wa Changsha.

Kufanikisha uwekezaji huo: “Super Agri watashirikiana na (Ukanda wa Uwekezaji wa Kilimo Tanzania) Tanzania Agricultural Export Processig Zone (TAEPZ).”

Makubaliano hayo yamefanyika leo, Juni 28, 2019 kati ya menejimenti ya kampuni hiyo na mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Lilian Ndosi na kushududiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi anayehudhuria mkutano baina ya taasisi za fedha za China na mawaziri 53 wa mambo ya nje kutoka Afrika.

Super Agri Technology itawekeza fedha hizo kwa kipindi cha miaka mitano.