Kanuni mpya za bima zazinduliwa

Muktasari:

Dk Saqware alisema inahitajika teknolojia rahisi na rafiki kwa ajili ya kusambaza, kununua, kuuza, kulipa mafao/madai ya bima na kusikiliza maoni na mahitaji ya wananchi, kuchakata na kuandikisha maombi ya huduma hiyo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (Tira) kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua kanuni za kutoa huduma za bima kupitia benki.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Yamungu Kayandabila aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo juzi, alizitaka taasisi za fedha nchini kuzingatia kanuni hizo katika utoaji wa huduma zao ili kuongeza ufanisi wa shughuli zao.

Alisema kanuni hizo zitasaidia kusambaza huduma za bima nchini kwani watu wengi bado hawajafikiwa.

“Ujio wa kanuni za kutoa huduma za bima kupitia benki nchini umechelewa kidogo hivyo wadau wana kila sababu ya kuzingatia kwa manufaa ya pande zote watoa huduma na wanufaika,” alisema

Alisema endapo wadau watazizingatia kanuni hizo, mapato katika sekta hiyo kiujumla yataongezeka kwa taifa na watoa huduma na watu wengi zaidi watafikiwa na huduma za bima.

Kwa upande wake, Kamishna wa Tira, Dk. Baghayo Saqware alisema licha ya manufaa lukuki ya kanuni hizo, pia zinalenga kuendeleza ajenda ya mamlaka hiyo ya kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za bima nchini yaani bima kwa wote.

“Tunahitaji kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za bima nchini kwa kuongeza aina mbalimbali za bima kwa mahitaji mbalimbali, mfano mbadala wa uuzaji na usambazaji wa huduma za bima ikiwamo kutumia benki,” alisema

Dk Saqware alisema inahitajika teknolojia rahisi na rafiki kwa ajili ya kusambaza, kununua, kuuza, kulipa mafao/madai ya bima na kusikiliza maoni na mahitaji ya wananchi, kuchakata na kuandikisha maombi ya huduma hiyo.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, kampuni za bima, taasisi za kifedha, mawakala na wadau wa sekta ya bima.