Kanyasu aagiza uhakiki mashamba yaliyovamiwa na tembo

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu

Muktasari:

  • Kutokana na baadhi ya watu kunufaika na fidia ya uharibifu wa mazao, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya  Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), kuchunguza uhalali wa malipo ya waathirika wa uvamizi wa wanyamapori walioharibu mazao yao

Bunda. Kutokana na baadhi ya watu kunufaika na fidia ya uharibifu wa mazao, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya  Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), kuchunguza uhalali wa malipo ya waathirika wa uvamizi wa wanyamapori walioharibu mazao yao.

Kanyasu ametoa agizo hilo leo Jumatatu Mei 27, 2019 mjini hapa alipokuwa anasikiliza kero za wananchi wa vijiji vya Sarakwa, Mariwanda, Unyalina na Kihomboi vinavyopakana na  Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wananchi hao wamemueleza Kanyasu kuwa licha ya mazao yao kuliwa, hawalipwi fidia badala yake wasiostahili ndiyo wananufaika na kifuta machozi kinachotolewa na Serikali.

Naibu waziri huyo amesema watakaobainika kunufaika na fidia zilizotolewa ilhali hawastahili, wachukuliwe  hatua kali za kisheria pamoja na kurudisha fedha walizopokea.

“Walipokea kifuta jasho au kifuta machozi wakati hawastahili, watazitapika,” amesema  Kanyasu.

Ili kuharakisha malipo ya fidia, naibu waziri amewakumbusha wananchi ambao mashamba yao yanavamiwa na tembo kutoa taarifa ndani ya siku tatu katika ofisi za kijiji ili hatua zikamilishwe kwa wakati.

Akitoa kero yake, mmoja wa wakulima waliozungumza kwenye ziara hiyo ya naibu waziri, Abel Hadawi amesema shamba lake lenye zaidi ya ekari 20 limeharibiwa mwaka jana lakini hajalipwa ingawa hali hiyo imejitokeza zaidi ya mara moja.

“Huu ni mwaka wa tatu najaza fomu lakini kila malipo yanapokuja jina langu huwa halimo,” amesema Hadawi.

Ingawa malipo hufanywa kwa mujibu wa sheria, wananchi hao wamemueleza naibu waziri kuwa fidia inayotolewa bado ni ndogo ikilinganishwa na gharama za kilimo zilizopo sasa hivi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Ziwa, Emmanuel Nkya amewaeleza wananchi hao kujaza fomu nne ili kuwe na nakala za kuanzia ofisi ya kijiji hadi makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Baada ya kuimarisha mikakati ya kudhibiti ujangili, tembo wameongezeka kwenye hifadhi za Taifa kiasi cha kuvamia makazi ya wananchi yakiwamo mashamba ambako uharibifu wa mazao hutokea.

Ripoti ya utakatishaji fedha na ugaidi ya mwaka 2016 (National money laundering and terrorism financing risks assessment report 2016) iliyotolewa hivi karibuni na Idara ya Udhibiti Fedha Haramu (FIU) ya Wizara ya Fedha na Mipango inaonyesha pembe za ndovu na faru ndizo zilizokuwa na bei kubwa zaidi kwenye soko la nyara hizo za Serikali.

“Ili kuzuia kutoweka kwa wanyama hao, kati ya mwaka 2011 na 2015, jumla ya matukio 4,161 ya ujangili yaliripotiwa na kesi 1,801 zikafunguliwa. Kati ya kesi hizo, 305 zilizowahusisha watuhumiwa 1,861 zilihukumiwa.

Ndani ya kipindi hicho pia, jumla ya watu 2,446, ripoti inasema walihukumiwa kwa kukutwa na nyara za Serikali baada ya ushahidi kushindwa kuthibitisha kujihusisha kwao na ujangili.

“Mara nyingi, ujangili unafanywa na wananchi wa kawaida ambao hulipwa fedha kidogo ikilinganishwa na wanayoipata wanaosafirisha kwenda nje ya nchi. Usafirishaji wa viungo vya wanyama hawa huratibiwa na mtandao mpana wa kihalifu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.