Kesi ya Zitto yakwama kuendelea mahakamani

Muktasari:

Kesi ya uchochezi inayomkabili Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe imeshindwa kuendelea leo Jumanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania kutokana na upande wa mashtaka kukosa kibali cha kuita mashahidi kutoka mkoani Kigoma.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imeshindwa kuendelea na usikilizaji wa kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazendo), Zitto Kabwe kutokana na upande wa mashtaka kukosa kibali cha kuita mashahidi kutoka mkoani Kigoma.

Wakili wa Serikali ya Tanzania Nassoro Katuga amedai hayo leo Jumanne Juni 18,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

"Kesi ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kipindi kilichopita tulieleza tunafuatilia mashahidi  Kigoma ambao kwetu ni muhimu tuliandika barua lakini Mfawidhi alisema kibali bado," amedai Wakili Katuga.

Kutokana na hatua hiyo, Wakili Katuga ameiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo wakati wakiendelea  kufuatilia kibali ili wapate mashahidi hao ambao wako sita.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 16 na 17, 2019.

Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwemo Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni John Makungu.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi ambapo anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.