Kesi ya mke wa Kisena yamsubiri DPP

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mke wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafiri wa Mabasi yaendayo Kasi (Udart), Robert Kisena, Florencia Mashauri umeieleza Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanategemea mabadiliko ya hati ya mashtaka kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mke wa aliyekuwa mkurugenzi wa Kampuni ya Usafiri wa Mabasi yaendayo Kasi (Udart), Robert Kisena, Florencia Mashauri umeieleza Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanategemea mabadiliko ya hati ya mashtaka kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Florencia ambaye ni mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil Gas Limited anakikabiliwa na mashtaka saba likiwamo la kuisababishia hasara kampuni ya Udart Sh 2,414,326,260.70.

Wakilli wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Imani Ntume jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile alieleza kuwa kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na wanategemea mabadiliko ya hati ya mashtaka kutoka kwa DPP..

"Tulikuwa tunategea mabadiliko ya hati ya mashtaka kutoka kwa DPP tunaomba ahirisho fupi kwa ajili ya kufanya mawasiliano na ofisi Yake" alisema Wakili Ntume.

Hakimu Rwizile aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 30 mwaka huu itakapotajwa tena na mshtakiwa alirudishwa rumande kutokana na makosa ya utakatishaji kutokuwa na dhamana.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa kati ya Januari 2011 na Mei 31 mwaka jana katika maeneo tofauti, mshtakiwa akiwa na watu wengine aliratibu shughuli za kihalifu huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kati ya Januari Mosi, 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani mshtakiwa akiwa mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil Gas Limited alijenga kituo cha mafuta kinachoitwa Zenon Oil and Gas katika karakana ya kampuni ya Udart bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma na Nishati na Maji (Ewura).

Katika shtaka lingine inadaiwa kati ya Januari Mosi, 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo alianzisha biashara ya kuuza mafuta ya petroli katika eneo ambalo hajaruhusiwa.

Katika shtaka la nne la utakatishaji fedha , inadaiwakati ya Mei 25, 2015 na Decembe 31, 2015 wakiwa jijini Dar es SAlaam mshitakiwa akiwa mkurugenzi wa Shirika la Usafiri  Dar es Salaam (UDA) aliiba Sh1,216,145 , 374 mali ya Udart.

Shtaka la tano, inadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa na lengo la kuficha uhalisia alibadilisha thamani ya mafuta kuwa fedha yenye thamani ya Sh.1.216, 145, 374 kwa kuyauza wakati akijua mafuta hayo ni zao la uhalifu.

Katika shtaka lasita,  anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 akiwa jijini Dar es Salaam kwa kumiliki Sh1.216, 145, 374 huku akijua ni zao la kosa za la wizi.

Katika kosa la saba inadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 akiwa jijini Dar es Salaam kwa makusudi aliisababishia hasara Udart ya Sh.2.414, 326, 260.70