Kibonde amfuata mkewe baada ya siku 240

Muktasari:

Mtangazaji wa Clouds FM, Ephrahim Kibonde amefariki leo Alhamisi Machi 7, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu


Dar es Salaam. “...kurudi kwa mwenyezi Mungu na kumkumbuka kwamba sisi binadamu hatuna lolote katika ulimwengu huu, kama si leo kesho, kama si kesho keshokutwa huwezi jua muda gani na siku gani wakati wako utafika safari yako itafika.”

Hii ni kauli ya Mtangazaji wa Clouds FM, Ephrahim Kibonde aliyoitoa hivi karibuni wakati akielezea kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.

Ruge alifariki duniani Februari 26, 2019 nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu kisha mwili wake ukarejeshwa nchini Machi 1, 2019 kisha ukazikwa Machi 4, 2019 kijijini kwao Kiziru, Bukoba mkoani Kagera.

Kibonde amefariki leo asubuhi Alhamisi Machi 7, 2019 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alipopelewa akitokea Bukoba katika mazishi ya Ruge baada ya hali yake kuibadilika.

Kifo cha Kibonde kimetokea ikiwa ni siku 240 zimetimia leo tangu alipofariki mke wake, Sarah Kibonde  kilichotokea Julai 10, 2018.

Sara alifariki katika katika Hospitali ya Hindu Mandal ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Kibonde kuonyesha bado anamkumbuka mke wake, Jumanne iliyopita ya Machi 5, 2019 alitumia akaunti yale ya Instagram ambapo aliposti picha ya mke wake kisha akaweka nukta tatu.

Posti  hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho hadi Kibonde ameondoka katika uso wa dunia.

Wachangiaji wa posti hiyo walitoa pole  na wale walioizungumzia leo wameonyesha kuguswa mathalani, official_elisha_isaya_jr amesema, “hii ni post yako ya mwisho tunatype sana kana kwamba utatujibu broo sijui ulikuwa unajua hii safari eeeh kifo hakuna anayeijua hii siri ya kifo aisee eeeh Mungu mpokee salama R I P.”

Naye mhando75 amesema, “Daah acheni Mungu aitwe Mungu.. Sijui alifikiria nini Kibonde kupost picha ya marehemu mke wake..jamani kumbe alikuwa anaona huenda wakaonana soon. R.I.P Kaka Ephraim Kibonde.”