Kibonde kuhitimisha safari yake duniani makaburi ya Kinondoni leo

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akimpa pole Ephrahim Kibonde Junior ni mtoto wa Marehemu, Ephrahim Kibonde alipofika nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach jijini Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Rais Magufuli amtumia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumfikishia salamu zake kwa wafiwa, ataja kipindi cha Jahazi alichokuwa akitangaza Kibonde kuwa kimekuwa kikimkosha zaidi

Dar es Salaam. Alikuwa akitumia zaidi ya robo saa kutoka anapoingia ndani ya geti la ofisi za Clouds Media Group mpaka kufika studio ilipo ghorofa tatu. Siyo kwamba alikuwa akitembea taratibu. Ephraim Kibonde alikuwa mtu wa watu, asipopita kumsalimia mtu, basi ataitwa kusalimiwa.

Ndivyo anavyomuelezea swahiba wake na mtangazaji mwenzake, Gadner G. Habash ambaye anasema kati ya mengi watakayoyakosa kwa kuondokewa na mwenzao huyo ni ukarimu wake.

“Ilikuwa huwezi kuongozana na Kibonde ofisini, utachoka, anaongea na kila mtu, yaani ninaweza kufika studio nikakaa zaidi ya dakika 20 yeye hajafika, yupo anaongea na watu,” anasema Gardner.

Kwa mara ya kwanza, ndani ya takribani miaka 20, wafanyakazi wa Clouds watamkosa baada ya leo kulazwa katika nyumba yake ya milele kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Gardner anasema Kibonde pamoja na ucheshi na wingi wa maongezi, kikubwa alichokuwa akipenda kuzungumzia ni watoto wake watatu.

Wakati ofisini wakilia kwa kumpoteza mwenzao waliyemtegemea, watoto wake watatu wamepigwa na butwaa kwamba mtu aliyechukua nafasi ya mama yao naye ameondoka. Mkewe Sarah alifariki dunia Julai 10, 2018. Mtoto wake wa kwanza, Ephraim Kibonde Jr anasema baba yake alimpigia simu mapema wakati akiwa Mwanza na kumwambia asiwe na wasiwasi kuwa angerejea siku iliyofuata.

“Sauti yake ilionyesha kuwa alikuwa akiumwa lakini naona alifanya vile kunitia moyo, aliniambia usiwe na wasiwasi ninakuja kesho, nililala nikiamini kuwa asubuhi atanipigia simu nimfuate uwanja wa ndege lakini nikashangaa naamshwa na taarifa za msiba,” anasema.

Dada yake aliyejitambulisha kwa jina la Lydia, anasema hata mara ya mwisho wakati wanazungumza jijini Mwanza alimuulizia kuhusu watoto.

Ingawa alikuwa amezidiwa alimuuliza kuhusu watoto lakini alikataa kuwasalimia kwa njia ya video ya simu (video call) na badala yake akamwambia atafanya hivyo akifika jijini Dar es Salaam.

“Nilipofika hali yake haikuwa nzuri, hata hivyo daktari aliniambia angalau alikuwa ameimarika kidogo. Niliongea naye na kwa kuwa alikuwa akiwaulizia watoto kila mara nilimwambia niwapigie simu ya video ili awasalimu na awape busu kwa kuwa walikuwa na wasiwasi,” anasema Lydia.

“Alinikatalia akasema hataki kuwapigia simu anataka kuwapa real kiss (busu la ana kwa ana), pia daktari alishauri kwa kuwa amechoka nimuache apumzike, nasikitika hakuweza kutimiza ahadi yake kwa watoto.” Kibonde ambaye ni mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha redio Clouds FM, alifariki dunia juzi alfajiri baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Rais Magufuli amlilia

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemwakilisha Rais John Magufuli kutoa salamu za pole katika msiba huo jana, alisema kifo cha Kibonde kimekuwa cha ghafla lakini mapenzi ya Mungu yametimia.

“Mimi nasimama hapa kwa niaba ya Rais John Magufuli, ameniagiza kuja kutoa salamu za rambirambi kwa kuwa yeye yupo na ugeni kutoka Rwanda. Kifo cha Ephraim Kibonde kimetustua sana. Tumemshuhudia Kibonde akifanya kazi vizuri kwenye mazishi ya Ruge. Nilipopata taarifa niliuliza mara mbilimbili ni kweli? Ila bado sote tuamini ni mapenzi ya Mungu” alisema Majaliwa.

Alisema kifo cha mtangazaji huyo kimemgusa Rais Magufuli ambaye ni msikilizaji na mfuatiliaji mzuri wa kipindi cha Jahazi ambacho Kibonde alikuwa akitangaza akishirikiana na Gardner na George Bantu.