Kigwangalla azungumzia bajeti yake kupita kiulaini

Wageni na wadau wa sekta ya Utalii na Maliasili waliotembelea bungeni wakimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangalla baada ya bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma juzi. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Tofauti na ilivyokuwa miaka minne iliyopita, wabunge bila kujali itikadi zao za vyama, juzi walipitisha bila vikwazo, bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2019/2020.

Katika mkutano wa bajeti wa mwaka jana na juzi, Maliasili na Utalii ilikuwa moja ya wizara ambazo bajeti zake zilizua mvutano bungeni, lakini safari hii wabunge wa vyama vyote walipongeza.

Tangu mwaka 1988 ni waziri mmoja tu wa Maliasili na Utalii, Zakhia Meghiji aliyedumu kwa muda mrefu kuiongoza wizara hiyo, akikaa kwa miaka minane kuanzia 1997 hadi 2005, wengine wamekuwa waking’olewa katika muda mfupi kwa sababu mbalimbali.

Ugumu wa wizara hiyo umekuwa ukijitokeza hata katika bajeti zake kwa wabunge kuwabana mawaziri kutokana na masuala kadhaa hasa ya kukithiri kwa ujangili na migogoro ya hifadhi na wananchi.

Dk Kigwangalla anaonekana kubadili upepo wa wizara hiyo baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo Oktoba 2017 na Rais John Magufuli.

Katika bajeti ya mwaka 2017/18, Kigwangalla alikutana na wakati mgumu kutoka kwa wabunge kuhusu mipaka ya hifadhi na vijiji hasa uwekaji wa vigingi hali iliyosababisha bajeti kupitishwa kwa mbinde.

Siri ya mafanikio

Nje ya viwanja vya Bunge juzi, jioni baada ya bajeti kupitishwa, Dk Kigwangalla aliiambia Mwananchi kuwa sababu ya kupitishwa kirahisi ni jinsi alivyozishughulikia changamoto zilizopo kwenye wizara yake.

“Nilipoteuliwa niliangalia changamoto za wizara hii. Mojawapo ni wananchi kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa, mifugo kuingia maeneo ya hifadhi na kuzidisha maeneo ya mipaka,” alisema.

Alisema ziara yake ya pori kwa pori ilikuwa ya kutatua shida alizokumbana na aliwashirikisha wabunge kwenye maeneo yao katika kila ziara.

“Leo hii kila mbunge anakuwa rafiki kwangu kwa sababu nimefika kwenye eneo lake na nimetatua changamoto ilioko katika eneo lake kwa hiyo anaona aibu kusimama hapa. Ndio maana umeona wachangiaji wote wanapongeza hakuna mchangiaji ambaye anapiga mawe,” alisema.

Alisema sababu nyingine ni uhusiano kati ya mawaziri na wabunge wenzake na kujishusha kila wakati.

“Ukijiweka juu wenzako watakuwa chini, wabunge wote ni sawa lakini kuna wengine wanakuwa mawaziri au wenyeviti wa kamati. Ukiwa unanyanyua mabega, wanakaa mbali wanakuchukia, wanaamua kukushughulikia kwa sababu ukiwa ndani ya Bunge unakuwa chini ya mamlaka ya wabunge kiitifaki,” alisema.

Alisema waziri anatakiwa kuwa mnyenyekevu na kuhakikisha anasikiliza zaidi kwani kufanya hivyo, anapata fursa ya kujifunza.

Alisema changamoto iliyokuwa ikimnyima usingizi na ambayo alipania kuitatua siku alipoteuliwa kuwa waziri ni mgogoro wa Loliondo, “hilo ndilo nilianza nalo. Ziara yangu ya kwanza ilikuwa ni Loliondo, si unaona kumetulia kule huo ni NGO, huoni wanaharakati wakipambana, huoni maboma yakichomwa moto huoni ng’ombe wakiuawa. Nimepatuliza. Ninaelewana vizuri na watu wa Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla,” alisema.

Alisema jambo jingine ni uwindaji wa kitalii ambao ulimfanya Rais Magufuli kumwekea ulinzi kwani huko kulielezwa kuwapo rushwa nyingi na kukosekana kwa uwazi.

“Baadhi ya mawaziri pia walikuwa wanasemwa wanafanya biashara ya chini ya meza na hao wenye vitalu. Lakini mimi nilipoingia nikasema nabadilisha mfumo naweka mfumo wa kugawa vitalu kwa njia ya mnada nikafuta vibali vilivyokuwepo,” alisema.

Alisema mnada wa kwanza wa vitalu utafanyika Juni kwa njia ya mtandao na kwamba hivi sasa wadau wa sekta hiyo wametulia.

“Kwa hiyo mwanzoni ulikuwa ni mgogoro mkali mpaka Rais akanipa ulinzi akanizuia kusafiri usiku na vitu kama hivyo lakini leo niko huru.

Lakini mimi sikutani na wafanyabiashara. Mimi sikai vikao mara mko baa wapi huko mnazungumza na wafanyabiashara,” alisema.

Wabunge waliochangia

Wabunge wengi waliochangia wakiwamo wa upinzani, walimpongeza Waziri Kigwangalla kwa kuibadili wizara hiyo.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa alisifia kuporomoka kwa ujangili akisema, “ujangili kweli umeporomoka. Nimekuweko katika wizara hii lazima tuwapongeze.”

Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini- Chadema) alimpongeza waziri huyo kwa programu maalumu aliyoanzisha ya ‘Tanzania unforgettable” akisema ipo katika viwango vya juu.

“Nilivyoiona nikasema sasa Kigwangalla yupo kazini lakini ‘take it international’ (ifanye iwe ya kimataifa) na wewe mwenyewe safiri nenda mamtoni ukazungumze nao wanataka nini uje uwaandalie,” alisema Sugu.

Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta aliipongeza wizara hiyo akisema imeanza vizuri.

Wengine walioimwagia sifa bajeti ya wizara hiyo ni Edward Mwalongo (Njombe Mjini-CCM), James Mbatia (Vunjo-NCCR Mageuzi) na mbunge wa Bunda (CCM) Boniface Getere.