Kilichojiri kesi ya Shamimu, mume wake hiki hapa

Mtuhumiwa  Shamim Mwasha na mumewe waaliokutwa na madawa ya kulevya wakipandishwa katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu kusomewa mashtaka  yao yanayowakabili. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha(41) wasubiri majibu ya kielelezo kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha (41) umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanasubiri majibu ya kielelezo kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Nsembo na Shamimu wakabiliwa na  shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini, kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,

Wakili wa Serikali Jenifer Massue, ameeleza hayo leo Jumatatu, Juni 10, 2019, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Massue ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina.

"Upande wa mashtaka kwa sasa tunasubiri majibu ya kielelezo kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi" Alidai Wakili Massue.

Massue amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, 2019 itakapotajwa na washtakiwa  wamerudishwa rumande.

Kwa mujibu  wa hati ya mashtaka, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 36/2019, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha  dawa za kulevya aina ya Heroini zenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Jijini Dar Es Salaam.

Kwa mara  ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Mei 13, 2019.