Kilimo fursa ya kuwa milionea

Licha ya kilimo kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, bado wengi waliojiajiri huko wana umasikini wa kipato. Wengi wanafanya kilimo cha kujikimu.

Tanzania hujitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100 kwa kila mwaka. Chakula hicho huzalishwa na wakulima wadogo ambao ni asilimia 80 ya wakulima wote.

Kilimo pia kinachangia uchumi kikiajiri karibu asilimia 67 ya Watanzania ambapo kati yao asilimia 65 ni wanawake.

Kilimo pia kinachangia asilimia 60 hadi 70 ya malighafi za viwandani na kinachangia asilimia 30 ya mapato ya nje na pato la ndani ni asilimia 25 hadi 30.

Licha ya mchango wote huo, bado wakulima ndiyo wanaowakilisha kundi la watu masikini nchini, huku kilimo chenyewe kikiwa na zana na teknolojia duni.

Kimsingi, bado wakulima wengi hawafaidiki na fursa za kilimo ambacho kama Watanzania watawekeza vilivyo huko, wanaweza kuwa mamilionea wakubwa.

Utafiti na uzoefu unaonyesha, ukiwekeza kwa dhati na kwa utaalamu, kilimo ni chanzo kizuri cha mapato. Ni kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau wameungana na kuwahamasisha Watanzania kujikitia katika kilimo kwa kuwapata tuzo.

Tuzo hizo zilikuwa na vipengele 16 ambavyo ni pamoja na biashara bora ya kilimo ya mwaka, mazao mchanganyiko ya biashara, biashara bora ya kilimo ya mwaka, biashara ya vifaa na mashine, wazalishaji wa chakula na vinywaji, Kundi la wanawake na mzalishaji bora wa matunda na mboga.

Vipengele vingine ni uwajibikaji bora wa jamii kwa mwaka, ubora kwenye elimu na mafunzo, ubora kwenye usafirshaji nje ya nchi, ubunifu katika kilimo, mashamba makubwa yenye mauzo ya zaidi ya Sh100 milioni, shamba dogo la mwaka (chini ya Sh100 milioni) na mwanamke bora katika kilimo.

Nyingine ni vijana bora katika kilimo, chipukizi kwenye biashara ya kilimo na biashara bora ya kilimo ya mwaka.

Akizungumzia tuzo hizo, Rais wa Chama cha Biashara, wenye viwanda na kilimo, Octavian Mshiu anasema lengo lake ni kukifanya kilimo kuwa rafiki kwa wawekezaji kwa kuwahamasisha kuwekeza zaidi.

“Hizi tuzo za kwanza zenye lengo la kuwahamasisha vijana na wote kwa jumla wajiunge na kilimo. Tunataka tukifanye kilimo kivutie,” anasema Mshiu.

Anaendelea; “Nimefurahi kuwaona watu ninaowajua na watu walioacha kazi zao na kujiunga na kilimo na kwa sasa sekta hii inaendelea kuwa chanzo kikubwa cha ajira nchini.”

Mshiu pia amempongeza Rais John Magufuli kwa kuhamasisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo, huku akiziomba halmashauri kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wanaotafuta ardhi kwa ajili ya kilimo.

Asilimia 44 ya ardhi ya Tanzania ndiyo inayofaa kwa kilimo lakini inayotumika ni chini ya asilimia 30 huku kukiwa na hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na maji ya kutosha yapo lakini ni chini ya asilimia tano ndiyo zinazomwagiliwa.

“Sekta binafsi ni mbia mkubwa wa kilimo, hata serikali ya awamu ya tano. Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutoa ardhi kwa wawekezaji. Kama Serikali ilivyoagiza kwa kila halmashauri itenge ardhi ya kilimo kwa wawekezaji itasaidia.

“Wawekezaji wakifika watapata ardhi. Wakiwekeza wataajiri wakulima wadogo kwa wingi na ndiyo jinsi ya kuongeza ajira,” anasema.

Hata hivyo, Mshio ameeleza kuwepo kwa malalamiko ya tozo kwa wakulima wa tumbaku akiitaka Serikali iangalie kero hiyo na kuitatua kwa manufaa ya viwanda vya Tanzania.

Unataka kuwa milionea?

Akizungumzia tuzo hizo, mdau wa kilimo, Dk Yusuf Sinare anasema mamilionea wa siku zinazo watatokana na sekta ya kilimo.

“Kama unataka kuwa milionea, ingia kwenye kilimo,” anasema.

Wakizungumza kuhusu tuzo hizo na maendeleo ya kilimo nchini, baadhi ya washindi wanasema licha ya kupambana kufikia mafanikio wanayopata, changamoto nazo hazikosekani.

Mshindi wa jumla katika mashindano hayo, Mkurugenzi wa Tomoni Farming Ltd, Franklin Bagala anasema kampuni yake imewekeza katika hekta 250 zilizopo kijiji cha Tomoni wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.

“Tunashirikiana na wanakijiji katika kilimo tukizalisha mananasi, maembe, machungwa, ndimu na mapapai,’’ anasema Bagala.

Kuhusu changamoto, Bagala anasema kuna changamoto ya kupata mikopo hasa katika Benki ya Maendeleo ya kilimo.

“Pamoja na riba ndogo ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo, lakini bado hatujaweza kupata mikopo. Bado tuko kwenye mazungumzo, kwa sasa tunapata mikopo ya benki za biashara,” anasema.

Bagala pia amezungumzia changamoto ya kutokuwepo kwa ujuzi katika matumizi ya teknolojia za kilimo, huku akishauri mitalaa ya shule za msingi na sekondari irejeshe soko la sayansi kilimo ili kuwawezesha wanafunzo kujenga uelewa wa kilimo wangali shuleni.

Maoni kuhusu mikopo ya TADB pia yametolewa na Elizabeth Swai ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya AKM Glitters Ltd akisema wamekuwa wakiwaombea mikopo wanachama wao bila mafanikio.

“Sisi tunafanya ufugaji wa kuku aina ya Kuroila kutoka India. Tunayo mashamba ya kuku wazazi, tuna kiwanda cha kutotolesha vifaranga, kiwanda cha vyakula vya kuku na tuna mradi wa maendeleo vijijini nchi nzima,” anasema Swai.

Anasema kupitia mradi huo wana mawakala 400 ambao huzunguka kutoa huduma za usambazaji wa kuku kwa wanavijiji zaidi ya 300,000.

Hata hivyo, linapokuja suala la kuwatafutia mikopo wafugaji, changamoto ndipo inapoanzia.

“Kupata fedha za TADB siyo rahisi, kwani tumejaribu kuwaombea wafugaji inaonekana, wakulima ndiyo wanapata kirahisi,” anasema.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine anasema ili mtu apate mikopo kwa urahisi ni lazima awe na mradi uliochanganuliwa vizuri.

Justine anasema tangu Julai 2017 benki hiyo imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh102 bilioni, ikiwa na miradi 84.

Kwa upande mwingine kampuni ya Taha Fresh ilipata tuzo ya ubora kwenye usafirshaji nje ya nchi. Mwakilishi wa kampuni hiyo, Fatuma Hussein anasema tuzo hiyo imetokana na uhamasishaji wao wa kusafirisha mazao ya mboga, matunda, maua na viungo nje ya nchi.