Kitendawili cha saa ya Nape

Dodoma. Tangu alipotangaza kujiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kutwa nzima ya jana, Nape Nnauye hakupokea simu alizopigiwa na waandishi wetu wakitaka ufafanuzi kuhusu hatua yake hiyo, lakini akaweka ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter uliojaa kitendawili.

Hatua yake hiyo ya kujiuzulu iliibuka hata bungeni jana baada ya Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga kudai kuwa kulitokana na shinikizo, kauli ambayo alilazimika kuifuta baada ya kushindwa kutoa ushahidi alipotakiwa kufanya hivyo na Spika Job Ndugai.

Licha ya mjadala huo ndani na nje ya Bunge, Nape hakupokea simu kuzungumza na Mwananchi, badala yake, mbunge huyo wa Mtama (CCM), kama alivyowahi kusema kwamba hupenda kuandika ujumbe unaofikirisha, aliweka katika akaunti yake ya Twitter picha ya saa ya mbao aina ya Kensington Station (789), bila ya kuongeza hata neno moja jambo lililoibua maswali mengi juu ya hatua hiyo.

Miongoni mwa maswali ambayo wadadisi walijiuliza ni kama; Je, alikuwa anamaanisha kwamba muda utazungumza, muda unakwenda, wakati ndio huu au ni suala la muda tu!

Hata alipochangia mjadala wa kamati yake jana jioni, Nape hakugusia suala la kujizulu kwake badala yake aliwataka wanasiasa wenzake kuweka akiba ya maneno wakati wanapowashutumu wenzao.

Akichangia taarifa ya kamati hiyo, Nape alisema kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama, anamshukuru Rais John Magufuli kwa kukubali maombi yao ya kufuta mashamba yaliyotelekezwa.

“Tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu. Wakati wa uchaguzi tulipeleka kwa Rais maombi ya kufuta baadhi ya mashamba yaliyotekelezwa,” alisema na kuongeza kuwa miongoni mwa mashamba hayo ni namba 37 lililopo Maumbika.

Ilivyokuwa bungeni

Suala la Nape kujiuzulu uenyekiti liliibuka bungeni wakati Haonga alipotoa taarifa akisema licha ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa ikiongozwa na Nape kusifiwa kwa kazi nzuri, imekuwa na utendaji mbovu ndiyo maana ameshinikizwa na kujiuzulu.

Hata hivyo, Haonga alilazimika kuondoa neno shinikizo katika taarifa yake baada ya kushindwa kuthibitisha hilo kama alivyotakiwa na Spika Ndugai lakini akasema mwenyekiti wao amejiuzulu bila kuwaeleza wajumbe.

Haonga alifikia hatua ya kumtaja Nape wakati wa mjadala wa taarifa ya kamati hiyo ambao awali, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ametaka kuundwa kwa kamati kuchunguza utaratibu uliotumika kunyang’anya mashamba hayo.

Akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Msigwa alisema licha ya kuwa haoni shida ya unyang’anywaji wa mashamba, lakini taratibu zinazotumika siyo sahihi.

Alisema kamati haikuweka baadhi ya mapendekezo kutokana ya kuitaka Serikali kuunda kamati ya kuchunguza jinsi unyang’anywaji wa mashamba hayo ulivyofanyika.

“Sina shida na unyang’anywaji wa mashamba kama ikifuatwa sheria na taratibu. Lakini kuna kitu ambacho nataka kusema wakati tupo kwenye kamati, kuna taarifa ambayo ilitakiwa iingizwe (kwenye taarifa ya kamati) lakini haikuingizwa,” alisema.

Alisema pamoja na sifa nyingi za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambazo alishawahi kumpa, suala hilo la mashamba makubwa lina harufu mbaya ya rushwa na ukakasi.

Hata hivyo, alikatishwa na taarifa kutoka kwa mbunge wa Simanjiro (CCM), James Ole Millya ambaye alisema, “Spika naomba nimpe taarifa mbunge anayeendelea kusema. Mimi natoka Jimbo la Simanjiro, takribani mwezi mmoja uliopita waziri alifuta mashamba zaidi ya 200… hakuna harufu yoyote wala asipende kumchafua waziri.”

Akiendelea kuchangia Msigwa alisema, “Nadhani unaenda haraka. Sijamchafua sasa ni wapi namchafua? Nimezungumza nimesema sina tatizo kabisa na mashamba makubwa kunyang’anywa kwa mujibu wa sheria na kufuata utaratibu.”

Alitoa mfano wa waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alidai alikuwa na shamba halali aliloliendeleza, “Mpaka ananyang’anywa shamba lake alikuwa na ng’ombe 200, kondoo 350, nyumba kubwa ya umwagiliaji, kisima, ghala la mazao, anaambiwa hajaendeleza nasema unyang’anyaji huu siyo sahihi, lakini najua kuwa Rais kubadilisha hati ana mamlaka hiyo Rais.”

Aligusia pia kunyang’anywa mashamba kwa mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji akisema lazima kamati ya kuchunguzi iundwe kuangalia hali hiyo.

Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere alimtaka Msigwa kuacha kusema uongo na kwamba kwenye kamati hawakuzungumza unyang’anywaji mashamba ya kina Sumaye lakini wamempongeza Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kutatua migogoro ya ardhi.