Kunywa dawa bila kufuata ushauri wa daktari husababisha ulemavu, kifo

Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Elizabeth Shekalage

Muktasari:

  • Ili dawa ifanye kazi mwilini, ina kiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi ya dawa aliyoandikiwa mgonjwa kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.

Dar es Salaam. Kwa sababu moja au nyingine wapo watu hunywa dawa nyingi bila maelekezo ya daktari ili wamalize dozi haraka.

Kuna  wanaokunywa vidonge vitatu vya maumivu badala ya viwili kwa kuzidiwa maumivu ya kichwa au tumbo ili wapate nafuu haraka, tofauti na maelekezo ya daktari.

Wengine pia, huenda kununua dawa bila kupata vipimo sahihi vya daktari ili kufahamu maumivu hayo yanasababishwa na nini.

Kuna wanaokunywa vidonge vitatu badala ya viwili kama walivyoelekezwa ili wapunguze siku za kunywa dawa, kama watatumia kwa siku 15 watumie kwa siku saba kwa sababu wanazozijua wao.

Msajili wa Baraza la Famasi nchini, Elizabeth Shekalage ameeleza madhara ya kufanya hivyo kuwa ni pamoja na kuleta ulemavu wa kudumu na hata kifo.

 Amefafanua kuwa ili dawa ifanye kazi mwilini, ina kiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi wa dawa aliyoandikiwa mgonjwa kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.

 Amesema mtu kunywa dawa zenye kiwango kikubwa (gramu)  ama chache tofauti na kinachotakiwa kulingana na ugonjwa uliopo kuna madhara mengi kiafya ikiwamo kifo.

Shekalage ameeleza kuwa upungufu dozi utasababisha ugonjwa kutokupona kutokana na kutotumia kiwango sahihi cha dozi kwa vimelea vya magonjwa na kutachangia kwa usugu wa bakteria kwa dawa husika.

Amesema kuzidisha dozi kunasababisha kuongeza kiwango cha dawa ambacho hakitakiwi kwenye mwili na huleta madhara ya figo, ulemavu na hata kifo.

 

Kwa undani wa habari hii usikose kusoma gazeti lako la Mwananchi kesho na ujifunze kuhusu usugu wa bakteria na madhara ya kunywa dawa tofauti.