Lissu amaliza matibabu, aandaa waraka mzito

Thursday January 3 2019

Tundu Lissu akiwa hospitalini huko Ubelgiji

Tundu Lissu akiwa hospitalini huko Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu. Picha na Maktaba. 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Tundu Lissu amehitimisha matibabu yaliyomchukua siku 480 baada ya kuondolewa vyuma vilivyokuwa katika mguu wake wa kulia ambavyo aliwekewa Julai 9, mwaka jana ili kuunganisha mifupa.

Baada ya kuhitimisha matibabu hayo yaliyotokana na majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mwaka juzi, mbunge huyo wa Singida Mashariki, amesema anatarajia kutoa waraka alioeleza umebeba ujumbe mzito juu ya masuala mbalimbali likiwamo tukio hilo na hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Lissu alisema alifanyiwa upasuaji wa mwisho wa kuondoa vyuma hivyo Jumatatu iliyopita mchana.

“(Upasuaji) ulichukua kama saa moja na nusu. Niliingia chumba cha upasuaji saa 6:30 mchana na nikatoka huko saa nane mchana.Baada ya hapo nilipelekwa chumba cha mapumziko kwa saa mbili za uangalizi halafu nikarudishwa chumbani kwangu saa 10:30 jioni.”

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji.

Hivyo, tangu Septemba 7, 2017 hadi Desemba 31, 2018, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametibiwa kwa kipindi cha siku 480 sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 24.

Akizungumzia hatua hiyo, mke wa Lissu, Alicia Magabe alisema, “Namshukuru sana Mungu kwa hatua hii na tunaanza kuona si muda mrefu tunarudi nyumbani ni furaha sana. Tumekuwa ugenini tangu Septemba 7 (2017) sasa tunapenda kurudi kuishi nyumbani kwa amani na kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki.”

Pia, kaka wa Lissu, Alute Mughwai alisema familia inamshukuru Mungu na, “Tunawashukuru sana Watanzania kwa jinsi walivyokuwa na sisi katika maombezi, michango ya hali na mali hadi sasa anapofikia hatua za mwisho za matibabu yake kwa kusimama mwenyewe.

“Lakini nawashukuru zaidi Hospitali ya Dodoma, Nairobi na Ubelgiji kwa jinsi walivyomhudumia,” alisema.

Alisema kwa kutambua mchango ulioonyeshwa na Hospitali ya Dodoma, familia ya Lissu imepanga kwenda kutoa shukrani maalumu.

Alipoulizwa kama familia hiyo itafanya hivyo katika hospitali nyingine alikolazwa, Alute aliyekuwa akizungumza kwa furaha alisema, “Tunaanzia nyumbani kwanza, ujue bila Hospitali ya Dodoma, Lissu asingefika Nairobi.”

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Ernest Ibenzi alipokea shukrani hizo za Alute na kusema ilikuwa moja ya kazi yao kuhakikisha wanaokoa maisha ya mgonjwa.

“Timu iliyomhudumia ilitekeleza wajibu wake ipasavyo hasa ikizingatiwa hali aliyokuwa nayo, kwa hiyo tunashukuru na wakiwa tayari tunawakaribisha,” alisema Dk Ibenzi.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu kauli ya Lissu kuhusu utayari wake wa kugombea urais mwaka 2020 iwapo vyama vya upinzani vitampitisha, Alute alisema familia haina tatizo na kwamba jambo la msingi kwao ni kuona ndugu yao anapona na anarejea nchini salama.

Aidha, Alicia ambaye kitaaluma ni mwanasheria alizungumzia nia ya mumewe kugombea urais alisema suala hilo ni litategemea mchakato ndani ya taasisi na ikiwa atapitishwa litakuwa jambo la heshima.
“Ni heshima na sifa na mimi nitamuunga mkono nikiwa mke wake, ubavu wake, msaidizi wake wa karibu sana kwa ngazi ya familia, mimi ni nani hadi nisimuunge mkono ikiwa taasisi zitamwamini? Nitamuunga mkono bega kwa bega,” alisema.

Desemba 26, mwaka jana, Lissu akizungumza na Mwananchi kuhusu ndoto zake za kuwania urais iwapo atapitishwa na vyama vya upinzani alisema, “Wakikaa katika vikao na kunipa bendera, nitakubali kubeba msalaba huo mzito kwa mikono miwili.”

Advertisement