Lissu asisitiza yupo tayari kwa Urais 2020

Tundu Lissu 

Muktasari:

Katika mahojiano yake na BBC, Lissu alisema kwamba nia yake ya kuutaka Urais haina maana kwamba anapambana na Lowassa lakini anaamini kwamba mapambano ya sasa yanahitaji nguvu zaidi.


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu ameendelea kusimamia msimamo wake kuwa yupo tayari kugombea urais mwaka 2020 endapo chama chake kitaona anatosha kusimama katika nafasi hiyo.

Akihojiwa na Shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) Lissu amesema kauli hiyo haina maana yoyote kwamba anapambana na Edward Lowassa ambaye alisimamishwa na Chadema mwaka 2015 kuwania nafasi hiyo.

“Kama chama changu pamoja na vyama tunavyoshirikiana navyo na Watanzania wanaotuunga mkono watasema kwamba mimi nafaa kuwawakilisha nitakuwa tayari kufanya hivyo.

Alisema, “Sina mpambano na Lowassa uamuzi wa kugombea urais sio wangu wala Lowassa wala Mbowe ni vikao vya chama. Inaweza kwenye vikao viongozi nikaambiwa sitoshi nitakubali na inawezekana vikao vikamwambia Lowassa aniachie mimi nipambane kwa sababu mapambano ya sasa yanahitaji nguvu inawezekana kabisa”.

Kuhusu kwamba ni lini atarejea nchini alieleza, “Daktari wagu atakaposema sasa una uwezo wa kurudi kwenu nitarudi Tanzania.

Lissu alieleza kuwa licha ya kwamba hadi sasa Serikali imeshindwa kufanya uchunguzi na kuwabaini waliomshambulia atarudi na itawajibika kumlinda kwa saa 24.

“Serikali inasema hao watu hawajulikani lakini bado hawajatafutwa, haujafanywa uchunguzi wowote ule hakuna aliyehojiwa, hawajajibu swali lolote, walinzi wa zile nyumba kwa nini siku ile hawakuwepo, hakuna anayeshukiwa, hakuna aliyehojiwa, hakuna uchunguzi sasa watawajuaje?

Serikali ya Rais Magufuli ambayo inasema haiwajui walionishambulia itakuwa na wajibu wa kuhakikisha saa 24 niko salama,” amesema.

Lissu ameweka wazi kuwa akipata nafasi hiyo atahakikisha nchi inakuwa na misingi imara isiyotegemea matakwa ya mtu binafsi.

“Tunataka nchi inayoheshimu uhuru wetu, haki za binadamu na Rais anayetambua kwamba neno lake sio kauli ya Mungu,” amesema.

Lissu alishambuliwa na risasi zaidi ya 30 mjini Dodoma, katika tukio lililotokea Septemba 7, 2017.