Lowassa: Mikutano ya hadhara ikiruhusiwa...

Muktasari:

  • Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani amefunguka kuhusu mikutano ya hadhara ikiruhusiwa kufanyika nchini Tanzania, atazunguka mikoani kuwashukuru wananchi waliompigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 
  • Lowassa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo nyuma ya Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema siku mikutano ya hadhara nchini Tanzania ikiruhusiwa kufanyika atakuwa wa kwanza kuzunguka mikoani kuwashukuru wananchi, wakiwemo waliompigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Ikifunguliwa nitakuwa wa kwanza kwenda mikoani kushukuru, isipofunguliwa nitawaachia nyinyi (wananchi) muamue Uchaguzi Mkuu utakapofanyika,” alisema Lowassa alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi.

Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu hali ya demokrasia nchini, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na nini maoni yake juu ya nafasi ya upinzani kueleza Uchaguzi Mkuu ujao.

Kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kumekuwa wimbo kwa wanasiasa wa upinzani, siku tatu zilizopita Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema zuio hilo ni changamoto kwa kuwa vyama vya siasa huhitaji kukua na kumea kila siku kupitia mfumo wa kuongeza wanachama wapya, jambo ambalo hivi sasa halifanyiki kutokana na marufuku iliyopigwa na Rais John Magufuli.

“Siasa za nchi ni nzuri kwa sababu watu wamechangamka kidemokrasia kudai haki zao na mambo yanafanyika mengi ya kutosha na yanayostahili sifa na yasiyostahili sifa,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli.

“Siasa katika nchi ni nzuri, lakini zinaweza kuwa nzuri zaidi kama Serikali ingekubali kuruhusu vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara, televisheni kutangaza mikutano ya Bunge.”

Alisema kuzuiwa kwa mikutano hiyo kunasababisha wabunge kufanyia siasa vichochoroni. Lowassa alitolea mfano kukamatwa kwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita mbaye pia ni diwani wa Vijibweni, Kigamboni.

“Naambiwa Mwita alifanya mkutano bila kibali amekamatwa na kuwekwa ndani. Amenisimulia nimesikitisha sana kutiwa ndani kwa kosa la kufanya mkutano katika mamlaka yake, hayo yanaharibu demokrasia,” alisema.

“Msingi wa demokrasia ni kuruhusu watu kusema maoni yao na unaweka heshima. Una maoni na mimi nina maoni tuheshimiane kwa maoni yetu hata kama ni sahihi au si sahihi lakini uniheshimu kwa maoni yangu.”

Alipoulizwa huenda wananchi wakawasahau wapinzani kutokana na kutokuwepo kwa mikutano hiyo, huku akitabasamu, Lowassa alisema, “Nasali sana watu wasitusahau…, nasali labda mikutano itafunguliwa karibuni. Wananchi wajue kuwa tulikuwa na nia ya kwenda mikoani kuwashukuru kwa kura zao.”

“Nakumbuka mapenzi ya wananchi Zanzibar, Tanga, Mtwara, Rukwa, Mbeya, Kagera, Mara na wengine walideki mpaka sehemu ya barabara tupite.”

Alisema anawakumbuka Watanzania wote waliokuwa na nia njema na yeye, na alitamani kuwashukuru lakini hakupata fursa hiyo.

Kuhusu nafasi ya upinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao alisema, “Nadhani mambo ni mazuri kwa sababu mambo ambayo Serikali ya Magufuli inayafanya tangu iingie madarakani ni makubwa yenye matatizo makubwa.”

Akifafanua madai kuwa amekuwa akimsifia Rais Magufuli, Lowassa “…,lazima niweke hili sawa kwamba sisi tungepewa nafasi tungefanya vizuri zaidi. Wale wanaonihukumu kwamba nampa sifa bila sababu, sifa zangu ziko qualified kwamba kama amefanya vizuri ingekuwa sisi wapinzani tungefanya vizuri zaidi.”

Alipoulizwa wangefanya nini tofauti na sasa alisema, “Vitu vingi tu kwa mfano sekta ya elimu, maji tungefanya vizuri zaidi.” Na alipotakiwa kueleza wangefanyaje alisema, “Hiyo ni ilani ya uchaguzi ya chama changu sihitaji kuieleza.”

Lowassa pia aligusia uchaguzi mkuu ujao na ule wa serikali za mitaa huku akisisitiza amani na utulivu na kutoa ujumbe kwa wanachama wa Chadema.

“Watanzania na wanachama wa Chadema uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu vinakuja. Tumekuwa na nchi yenye amani na utulivu, nawaomba wakubwa waliopo madarakani kuendeleza umoja na mshikamano ili mambo yaendelee kwenda vizuri katika nchi,” alisema.

“Lipo jambo la pili kwa chama changu, tulikaribia goli wakasema hatukukaribia, tulifunga goli wakasema hatukufunga anajua Mwenyezi Mungu kilichotokea.”

Alisisitiza, “Lakini napenda kuwaomba tujipange vizuri kwa Uchaguzi Mkuu na wa serikali za mitaa. Tuwe wamoja, tukiwa wamoja tutawashinda vyama vingine, tukianza maneno ya chinichini na tusipokuwa wamoja itakuwa si vizuri. Tutashinda tukienda kwa umoja wetu na kuacha maneno ya kugombana kila mahali na kila saa.”