Lowassa na funzo la akiba ya maneno

Muktasari:

  • Kuhama kwa Lowassa kipindi hiki kunastahili pongezi kwa sababu ametoa fursa mapema kwa Chadema kujipanga upya bila ya kutegemea kwamba yeye yupo.

Matukio ya kisiasa yameanza kutikisa nchi kuelekea uchaguzi mkuu mwakani. Juzi tumeona Maalim Seif akihamia ACT-Wazalendo na hivi karibuni tulishuhudia Edward Lowassa akitangaza kurejea CCM kwa maneno mawili tu “narudi nyumbani”.

Lowassa alitamka maneno hayo akimaanisha kwamba ameamua kuhama chama kilichompa fursa kutimiza kiu yake ya kugombea urais mwaka 2015 na kupata kura zaidi ya milioni sita.

Binafsi nampongeza Lowassa kwa mambo matatu, mosi, namna alivyochagua muda wa kuhama kutoka Chadema kwenda CCM licha ya kuwapo watu wanaomlaumu kwamba amehama wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa mahabusu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba mwanasiasa huyo angeamua kukaa Chadema hadi uchaguzi mkuu ujao angeweza kukivuruga chama hicho kikuu cha upinzani.

Kuhama kwa Lowassa kipindi hiki kunastahili pongezi kwa sababu ametoa fursa mapema kwa Chadema kujipanga upya bila ya kutegemea kwamba yeye yupo.

Ni wazi kwamba kuwapo kwa Lowassa ndani ya Chadema kungekuwa ni mtihani mkubwa wakati wa kumpata mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu mwakani.

Kura 6.2 milioni alizopata Lowassa zilionesha ni jinsi gani alivyo mzito kwa siasa za Tanzania, hivyo jambo hilo lingewawia vigumu kumuweka pembeni katika urais wa 2020.

Kwa maana hiyo binafsi naona Lowassa aliona mbali na hakutaka kuudhoofisha upande wa Chadema na Ukawa uliompokea na kumpa heshima kubwa mwaka 2015.

Jingine ni namna alivyoweka akiba ya maneno wakati wa kuzungumza pale Lumumba alipopewa nafasi hakusema mengi zaidi ya “narudi nyumbani”. Watu wa upinzani wanashindwa kumshambulia Lowassa kwa kitendo chake cha kuhamia CCM kwa sababu hakuna lolote baya alilolisema zaidi ya kuweka akiba ya maneno.

Hivi makada wa CCM waliokuwa wakimtukana na kumvunjia heshima yake mwaka 2015 wataweka wapi sura zao watakapokutana naye uso kwa uso?

Pia kuna funzo jingine kwamba kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu, ndiyo maana siku chache zilizopita, Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga alipinga kwa nguvu zote kutangazwa kwa Uhuru Kenyata kuwa Rais wa Kenya hadi akafikia hatua ya kujiapisha lakini leo ni rafiki wa Rais Kenyatta.

Wahenga hawa wametufundisha kwamba ni bora kujenga tabia ya kuweka akiba ya maneno kuliko hata chakula na fedha.