Lugola aagiza maofisa polisi mkoani Geita kusimamishwa kazi

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametoa siku mbili kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasimamisha kazi mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, kaimu mkuu wa upelelezi  na mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo kwa kutowachukulia hatua askari waliosababisha mahabusu kutoroka

Geita. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametoa siku mbili kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasimamisha kazi mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, kaimu mkuu wa upelelezi  na mkuu wa kituo cha polisi wilayani humo kwa kutowachukulia hatua askari waliosababisha mahabusu kutoroka.

Pia, ameagiza kukamatwa askari wanane waliokuwa lindo mahakamani ya wilaya hiyo kwa kufanya uzembe na kusababisha mahabusu kutoroka.

Mei 21, 2019 mahabusu 15 wanadaiwa kutoroka wakati wakisubiri kuitwa kwa ajili ya kesi zao.

Imeelezwa kuwa mahabusu hao walifungua mlango wa nyuma wakati askari wakiwa nje ya lango kuu la kuingia katika ukumbi walikokuwa wamewekwa. Hadi sasa mahabusu wanne wameshakamatwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 24, 2019 Lugola amesema mahabusu waliotoroka walikuwa wakikabiliwa na kesi za mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, uhujumu uchumi na makosa mengine.

Lugola amesema kitendo cha mahabusu kutoroka wakiwa mahakamani kimelitia doa  Jeshi la Polisi na kwamba taasisi hiyo itaendelea kuheshimiwa na askari atakayesababisha uzembe au kufanya kosa ataondolewa kwa fedheha.