Lugola asitisha ziara Rukwa, atimukia Morogoro

Saturday August 10 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola 

By Mussa Mwangoka, Mwananchi

Sumbawanga. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amefuta ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Rukwa kufuatia msiba mkubwa uliolikumba taifa.

Ziara hiyo ilikuwa ianze leo Jumamosi Agosti 10, 2019 ambapo angetembelea wilaya zote za mkoa huo lakini ajali ya lori lililotokea leo asubuhi Msamvu mkoani Morogoro na kuua watu 64 na majeruhi zaidi ya 70 imemfanya waziri huyo kusitisha ziara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Rukwa, Waziri Lugola amesema amehirisha ziara hiyo.

Amesema si busara kuendelea na ziara ya kukagua shughuli za utendaji wa idara zilizopo chini ya wizara yake wakati taifa limekumbwa na msiba mkubwa watu wengi uliotokea mapema leo asubuhi mkoani Morogoro.

"Tumepata msiba mkubwa kama taifa na mimi ndiye waziri ninahusika na wizara hiyo, sasa siwezi kuendelea na ziara hapa Rukwa nakwenda Morogoro sasa hivi (ilikuwa mchana) ili kusaidiana na wenzangu wa wizara nyingine ili kuona namna ya kuwasaidia wenzetu ambao wamepata majeraha ya ajali hiyo," amesema Waziri Lugola

Amesema akiwa Morogoro pia atatoa maelekezo ya nini kifanyike ili kupunguza ajali kama hizo ambazo zinapoteza vifo vya watu wengi.

Advertisement

Naye, Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amesema kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Rukwa amepokea kwa masikitiko msiba huo na anatoa pole kwa ndugu na jamaa waliopoteza ndugu zao huku akiwaombea majeruhi wapone haraka na kurejea katika kazi zao za ujenzi wa taifa.

Advertisement